Na Saulo Steven – Singida.
Mamlaka ya udhibiti wa huduma za Nishati na Maji (EWURA), Kanda ya kati imewataka wakazi mkoani Singida kuhakikisha wanatumia Nishati safi ya kupikia kwa usalama na kuzingatia matumizi sahihi ya nishati hiyo (Gesi).
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa EWURA kanda ya kati, Bi Hawa Luweno, wakatia akiongea kwenye semina ya siku moja juu ya matumizi sahihi ya Nishati safi iliyofanyika katika ukumbi wa RC mission mjini Singida.

Ambapo amesema lengo la kutoa elimu hiyo kwa wakazi wa mkoa wa Singida nikutokana na baadhi ya Wananchi kutokuwa na elimu sahihi juu ya matumizi ya nishati safi hali ambayo imekuwa ikileta madhara yasiyotarajiwa ,hivyo EWURA imeahidi kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu matumizi ya nishati ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa ajili ya Afya ya jamii na uhifadhi wa Mazingira.

Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa Singida, walioshirika katika mafunzo hayo ya matumizi sahihi ya Nishati safi baadhi wameishukuru EWURA kwa kuandaa semina hiyo na kuomba elimu hiyo isambae hadi vijijini ambako bado kuna uelewa mdogo wa matumizi salama ya gesi ya kupikia.
“Tumejifunza mambo muhimu sana kuhusu usalama wa mitungi yetu na matumizi ya gesi majumbani,Tunaiomba EWURA iende mbali zaidi, hasa vijijini ambako watu bado wana wasiwasi kutumia gesi,” alisema mmoja wa washiriki katika mafunzo hayo.