Kongamano linaloungwa mkono na Umoja wa Mataifa limeahidi karibu dola milioni 630 za kuushughulikia mzozo wa kiutu nchini Ethiopia, jumla ya nchi 21 zikiongozwa na Marekani iliyoahidi dola milioni 253 zimetoa ahadi mpya kulisaidia taifa hilo.
Kiasi hicho hata hivyo hakijafikia dola bilioni moja zinazohitajika ili ilikuwalisha mamilioni ya watu wanaokabiliwa na mizozo na mabadiliko ya tabianchi katika nchi hiyo ya pili kwa idadi kubwa ya watu barani Afrika na naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya Kibinadamu Joyce Msuya amesema katika kuwa mchango huo ni mwanzo tu na wanatumaini kuendelea kuonesha uungaji mkono kwa mwaka mzima.
Mkutano huo wa wafadhili ulioandaliwa katika makao kuu ya Umoja wa Mataifa barani Ulaya jijini Geneva unataka kuchangisha fedha ambazo taasisi hiyo ya kimataifa inasema zinahitajika haraka ili kushughulikia msaada kwa miezi mitatu ijayo.
Uingereza ambayo ilikuwa mwenyeji mwenza wa mkutano uliofanyika jana, iliahidi dola milioni 125, huku Umoja wa Ulaya ukisema kwa pamoja na nchi wanachama utatoa zaidi ya dola milioni 139.
Waethiopia wanakabiliwa na migogoro ya ndani wakati kukiwa na athari za kiuchumi na mabadiliko ya tabia nchi na mzozo unaozidi kuwa mbaya wa chakula na utapiamlo, Uingereza imesema Ethiopia inakabiliwa na hatari ya kufunikwa na migogoro mingine ya kibinaadamu.
Marekani pia imesema kuwa inatoa dola milioni 154 za msaada wa kiutu ili kuyashughulikia mahitaji ya dharura yatokanayo na mzozo, ukosefu wa usalama na athari za mabadiliko ya tabia nchi. Wafadhili pia wameitaka serikali ya Ethiopia kuhakikisha utoaji wa misaada bila kuingiliwa.
Mwaka jana Shirika la Maendeleo ya kimataifa la Marekani lilisimamisha misaada yote ya chakula kwa Ethiopia kwa miezi kadhaa baada ya uchunguzi wa ndani kubaini kuwepo kwa uporaji mkubwa.