Jeshi la Polisi mkoa wa Mtwara, limewaomba ndugu na jamaa wa Anastanzia Exavery Mahatane (27) maarufu kama Ebitoke, ambaye alichapisha taarifa za kutekwa na kutumbukizwa katika shimo hivi karibuni, kufika Mkoani humo kutoa msaada au kumchukua ndugu yao.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Mtwara iliyotolewa hii leo Agosti Mosi, 2025 imeeleza kuwa Julai 31, 2025 lilimkamata Ebitoke katika fukwe za Msanga Mkuu, akiwa katika hali inayoonekana kuwa amechanganyikiwa na si kama alivyoeleza katika mitandao ya kijamii.

“Anastanzia Mahatane alichapisha taarifa katika akaunti zake za mitandao ya kijamii ikiwemo Instagram kuwa yeye kwa sasa yupo Mtwara na kwamba ametumbukizwa katika shimo huko katika fukwe za Msanga Mkuu na kwamba wapo watu ambao aliwataja kwa majina kuwa wanataka kumuua,” ilielezwa.
Kufuatia taarifa hiyo, Jeshi la Polisi Mkoani Mtwara lilianza uchunguzi wa haraka ili kujua ukweli wa taarifa iliyotolewa na Ebitoke na kubaini kuwa alifika mkoani Mtwara tangu Aprili 2025 na kufikia hoteli moja iliyopo Msanga Mkuu kuomba hifadhi kwa watu waliokuwa wanafahamiana kabla ya maisha yake
kumuendea vibaya.
Kwasasa Anastanzia Exavery Mahatane (Ebitoke), amefikishwa katika Hospitali ya Mkoa wa Mtwara kwa ajili ya matibabu.

