
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ni kiongozi bora barani Afrika kutokana na mageuzi makubwa aliyoyafanya nchini, ambayo yamepongezwa si tu na Watanzania bali pia na taasisi mbalimbali za kitaifa na kimataifa.
Akizungumza katika mdahalo wa Mafiga Manne ya Samia uliofanyika mkoani Mwanza Jumanne, Machi 18, 2025, Majaliwa ameeleza kuwa Rais Samia ameimarisha uchumi wa nchi, demokrasia, utawala bora na maendeleo ya jamii, hatua ambazo zimemfanya kutambuliwa kwa heshima kubwa ndani na nje ya Tanzania.
“Ninataka niwaambie, Rais wetu huyu, kwa haya aliyoyafanya ndani ya nchi, hatujampongeza sisi Watanzania tu, ndiyo muone kuwa tuna Rais bora kabisa Afrika. Amepongezwa na taasisi mbalimbali hapa nchini ambazo pia zimeweza kutoa nishani mbalimbali kwa mageuzi makubwa ya kiuchumi aliyoyafanya, ameimarisha misingi ya demokrasia, utawala bora na maendeleo ya jamii,” amesema Waziri Mkuu.
Ametaja baadhi ya vyuo vikuu vilivyotambua mchango wa Rais Samia, ikiwa ni pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru nchini India, na Chuo Kikuu cha Ankara nchini Uturuki, ambavyo vimemtunuku tuzo za heshima kutokana na uongozi wake.
Aidha, ameeleza kuwa Rais Samia amepata kutambuliwa kimataifa, akitaja jarida maarufu la Forbes lililomtangaza mara tatu mfululizo kuwa ni Rais bora mwanamke barani Afrika, kiongozi shupavu na mwenye ushawishi mkubwa. Pongezi kwa Rais Samia zimeendelea, ambapo hivi karibuni, tarehe 4 Februari 2025, Taasisi ya Gates Foundation ilimkabidhi tuzo ya kimataifa ya The Global Goalkeepers Award kwa kutambua juhudi zake katika sekta ya afya.