Uchunguzi wa kutumia vinasaba, DNA unatarajiwa kuanza leo nchini Kenya kusaidia kuwatambua wanafunzi waliopoteza maisha katika mkasa wa moto kwenye shule ya Hillside Endarasha katika kaunti ya Nyeri, wiki iliyopita.
Watoto hao walifariki dunia Alhamisi ya wiki iliyopita(Septemba 5,2024) baada ya moto kuteketeza bweni lao katika shule hiyo ya Hillside Endarasha walipokuwa wamelala kabla ya Jumamosi ya Septemba 7,2024 msemaji wa serikali Isaac Mwaura, kusema miili 19 ilipatikana kwenye magofu yaliyoteketea ya jengo hilo, huku wanafunzi wengine wawili wakifia hospitalini, na 17 wakiwa hawajulikani waliko.
Polisi imesema miili ya wanafunzi hao, wenye umri wa kati ya miaka 9 na 13, iliteketea kiasi cha kutotambulika, na familia zimekuwa na wakati mgumu kusubiri kujua hatma ya wapendwa wao.
Hapo jana(Jumapili ya Septemba 8,2024) kamishna wa kaunti ya Nyeri Pius Murigu, aliliambia shirika la habari la AFP kwamba shughuli ya kitaalamu ya kufanyia uchunguzi miili hiyo itaanza leo kwa sababu hiyo ndio njia ya pekee miili hiyo inaweza kutambuliwa.
Murigu alizihimiza familia zilizoathirika kujitokeza leo katika hospitali ya Naromoru na kushiriki katika mchakato unaofuata wa utambuzi huo wa kitaalamu wa mabaki ya miili ya wanafunzi hao kutokana na janga hilo.
Kwa upande wake mtaalamu mkuu wa upasuaji maiti wa serikali, Johansen Oduor amesema walifanikiwa kuipata miili 19 ambayo imeungua sana kiasi kwamba isingewezekana kwa wazazi wao kuweza kuitambua.
Hata hivyo, Oduor amesema upasuaji wa maiti kwa uchunguzi utaanza Jumanne ya Septemba 10 na hivi sasa Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Kenya limeendelea kutoa ushauri wa kisaikolojia kwa watoto na jamaa waliopatwa na kiwewe, huku wakiweka mahema meupe nje ya lango la shule hiyo ya Endarasha.
Tukio hilo la Alhamisi limeangazia suala la usalama katika shule nchini Kenya, baada ya kutokea visa vingi sawa na hicho katika miaka ya nyuma vingi vikiwa vibaya mno,kabla ya kupoa kwa maumivu ya tukio hilo Jumamosi usiku(Septamba 7,2024) moto mwingine ulizuka katika shule ya sekondari ya wasichana ya Isiolo pia katika eneo la Kati mwa Kenya huku picha zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zikionesha majengo mengi yakiteketea.
Mkurugenzi wa mawasiliano katika kaunti ya Isiolo Hussein Salesa, ameiambia AFP kwamba kulikuwa na majeruhi kadhaa, lakini polisi inasema hakuna aliyejeruhiwa.
Hapo jana Jumapili, moto mwingine uliteketeza bweni katika shule ya sekondari ya wavulana ya Njia katika kaunti ya Meru wakati wanafunzi walipokuwa wakila chakula cha jioni na kulingana na taarifa ya polisi hakuna majeruhi walioripotiwa katika tukio hilo.