Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan amewataka vijana nchini kuulinda Muungano na kukumbuka kuwa Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar ni tunu ya Taifa na Afrika kwa ujumla na kuwasihi wanasiasa kudumisha mafanikio yaliyopatikana katika miaka 60 ya Muungano huu kwa kudhamiria kufanya siasa zenye kuleta Maendeleo,kuunganisha watu,kuheshimiana na kudumisha Misingi ya Utawala wa Sheria.
Rais Samia ameyasema hayo hii leo (April 25,2024) kupitia hotuba yake ya Miaka 60 ya Muungano ambapo pia ameelezea mafanikio mbalimbali yaliyopatikana nchini katika kipindi chote tangu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulipoasisiwa.
Akizungumzia mafanikio katika Sekta ya Mawasiliano,Rais Dkt. Samia amesema kwamba mawasiliano ya vyombo vya habari,simu na mitandao ya kijamii vimeimarika ambapo laini zipatazo milioni 72 za simu zinatumika,nchin ikiwa watoa huduma za mawasiliano watano amabo hivi sasa wanatoa huduma ya kasi ya 5G, pamoja na uwepo wa laini za simu milioni 53 zinazotumika katika huduma za kifedha kupitia simu za mkononi.
Aidha amebainisha kwamba asilimia 98 ya Watanzania wanafaidika na huduma za Mawasiliano katika kipindi ambacho kupitia mfuko wa Mawasiliano kwa wote ulioanzishwa mwak 2009, mawasiliano yameweza kufikishwa kwa Watanzania milioni 16 kutoka katika kata 1,306 na vijiji 3,838 vimefikiwa na mawasiliano ya uhakika.
Rais Dkt.Samia ameyataja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na kuimarishwa kwa uhuru wa kujieleza,mabadiliko ya Sheria mbalimbali kama vile ,Sheria ya Uchaguzi, Sheria ya vyama vya Siasa,kupitiwa kwa mfumo wa hakijinai,kutambuliwa kwa haki za binadamu na kuanzishwa kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora na mihimili mitatu ya Dola kutekeleza Majukumu yake bila muingiliano.
Aidha amebainisha mafanikio mengine ya miaka 60 ya Muungano kuwa ni Tanzania imeweza kuwa na Ushawishi mkubwa kikanda na kimataifa hali iliyopelekea kukuza uhusiano baina ya nchi yetu na nchi nyingine na Taasisi za Kimataifa kwa manufaa ya pande zote mbili za Muungano pamoja na kuvutia mitaji ya Uwekezaji,Teknolojia na kupata soko la bidhaa na huduma.