Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi ameiagiza Menejimenti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ( TPA) kuhakikisha Mradi wa Usanifu na Ujenzi wa Bandari mpya wa Mbamba Bay iliyopo Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma unakamilika kwa wakati na kwa ubora.
Akizungumza tarehe 05 Aprili,2025 baada ya kutembelea na kukagua mradi huo mkubwa na wa kimkakati, Mhe. Balozi Nchimbi amesema kukamilika kwa Bandari ya Mbamba Bay, kutaimarisha zaidi Biashara katika mikoa ya kusini na nchi Jirani za Malawi na Msumbuji.

Balozi Nchimbi pia ameipongeza Menejimenti ya TPA kwa kuusimamia vyema Mradi huo muhimu na wa kimkakati ambao anasema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatoa umuhimu wa pekee katika kukamilika kwake.
Mapema akitoa maelezo ya mradi huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu Bw. Plasduce Mbossa, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA Dkt. Baraka Mdima, amesema mradi huo utakaojengwa kwa miezi 24, unatarajia kukamilika kwa wakati kwa mujibu wa mkataba.