Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amewataka Watanzania kuibua taarifa zinazohusu vitendo vya ukatili, ili hatua stahiki zichukuliwa dhidi ya wahusika.
Dkt. Mpango ametoa wito huo hii leo Januari 20, 2025 jijini Arusha, alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Maadhimisho ya Miaka 25 ya Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA).
Amesema, wapo Wanawake, Watoto na Wanaume wanaopitia vitendo vya ukatili wa kijinsia au kimwili lakini hawatoi taarifa kwenye vyombo vya sheria na kwamba baadhi ya mila na desturi zimekuwa zikitumika kuwakandamiza waathirika.

Makamu wa Rais ameongeza kuwa pamoja na dhamira njema ya Serikali ya kuhakikisha usawa wa kijinsia hapa nchini, bado wanawake ambao idadi yao ni zaidi ya nusu ya watu hapa nchini, wanapewa nafasi ndogo katika umiliki wa mali na wanabaguliwa kwa msingi wa jinsia.
Aidha, amesema kwa mujibu wa Mpango wa Kitaifa wa Kupinga vitendo vya Kikatili dhidi ya Wanawake wa mwaka 2016, kati ya wanawake kumi, wanne wamepitia ukatili wa kimwili, na mmoja kati ya watano wamepitia ukatili wa kingono miongoni mwao wakiwa na umri mdogo (chini ya miaka 15).
Kulingana na Ripoti ya UN Women Social Institution and Gender Index (SIGI) 2022, ukatili wa kijinsia nchini Tanzania unabainishwa zaidi kupitia ndoa za utotoni, ubaguzi ndani ya familia, ukatili dhidi ya wanawake, ukosefu wa uhuru katika kupanga uzazi, upatikanaji na umiliki wa ardhi.

Aidha,taarifa ya tathmini ya Ukatili wa Kijinsia Tanzania iliyoandaliwa na Benki ya Dunia mwaka 2022, asilimia 40 ya Wanawake wote wenye umri wa miaka 15 hadi 49 wamefanyiwa ukatili wa kimwili na asilimia 17 wamepitia ukatili wa kingono.
Hata hivyo, Makamu wa Rais amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imejizatiti kuimarisha usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake hapa nchini kwa kuanzisha Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ambayo inasimamia masuala ya usawa wa kijinsia.
Amesema dhamira hiyo ya Serikali inaonekana zaidi kupitia mikakati, mipango na sera za kitaifa kama vile Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, Mipango ya Maendeleo ya Taifa ya Miaka Mitano, Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (NSGR) na Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya 2000.

Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma ameishukuru Serikali kwa dhamira njema na kuendelea kuiwezesha Mahakama ambapo Majaji wa Mahakama ya Rufani wameongezeka kutoka Majaji 17 mwaka 2021 hadi Majaji 40 mwaka 2025.
Prof Juma amesema ni jukumu la Majaji na Mahakimu kuitumia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 ili kufikia malengo yaliyotajwa ikiwemo vipengele vyote vinavyotaja masuala ya kijinsia na kisheria.

Awali akitoa taarifa, Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Barke Sehel amesema mafaniko yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 25 ya TAWJA yanatokana na mifumo imara ya usawa kijinsia hapa nchini pamoja na ushirikiano mzuri kutoka katika Serikali na Mahakama ya Jamhuri ya Tanzania na Mahakama ya Zanzibar.
Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) kilianzishwa mwaka 2000 ambapo kinasherehekea Jubilei ya miaka 25 yenye kauli mbiu isemayo “Jubilei ya Miaka 25 ya TAWJA: Kusherehekea Utofauti na Mshikamano katika Usawa wa Kijinsia” Imetolewa naOfisi ya Makamu wa Rais20 Januari 2025Arusha.