DKT. LEBBA ATAKA WANANCHI KUWA SEHEMU YA SULUHISHO MAPAMBANO DHIDI YA KIFUA KIKUU, UKOMA

Na Saulo Stephen – Singida.

Wananchi mkoani Singida wametakiwa kuwa sehemu ya suluhisho katika mapambano dhidi ya Kifua Kikuu na Ukoma kwa kushirikiana na wataalamu wa afya katika kuibua wagonjwa, kuhakikisha wanapata huduma kwa wakati na kufuatilia matibabu yao hadi kukamilika.

Wito huo umetolewa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Jesca Lebba, wakati akifungua Kikao cha Mapitio ya Takwimu za Nusu Mwaka za Kifua Kikuu na Ukoma kilichofanyika katika Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Singida.

Dkt. Lebba amesema kikao hicho kinalenga kupitia mwenendo wa takwimu za magonjwa hayo, kutathmini utekelezaji wa viashiria muhimu, kubaini changamoto na kuweka mikakati ya kuboresha huduma kwa wananchi.

Amesema wataalamu wa afya wanapaswa kuendelea kuwaibua wagonjwa wa Kifua Kikuu na Ukoma katika jamii na kuhakikisha wanapatiwa huduma stahiki kwa wakati, ili Mkoa uweze kufikia lengo lililowekwa la asilimia 80 katika utambuzi na utoaji wa huduma kwa wagonjwa.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwa na takwimu sahihi na zenye ubora, huku akiwataka wataalamu kuimarisha uchunguzi kwa wagonjwa wanaofika katika vituo vya kutolea huduma za afya, ili wenye dalili au viashiria vya magonjwa hayo waweze kutambuliwa mapema na kupewa matibabu kwa wakati.

Dkt. Lebba amesema ufuatiliaji wa karibu kwa wagonjwa wanaopata matibabu ni muhimu katika kuhakikisha wanakamilisha dozi zao na kupunguza uwezekano wa maambukizi mapya, hivyo kuwataka wataalamu wa afya kuwafikia wagonjwa kwa ukaribu na kuhakikisha huduma zinatolewa kwa ufanisi.

“Kila mmoja wetu awe sehemu ya suluhisho,” amesema Dkt. Lebba, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wataalamu wa afya, wananchi na wadau mbalimbali katika kuimarisha mapambano dhidi ya Kifua Kikuu na Ukoma.

Sambamba na hilo, amewataka wataalamu wa afya kuendelea kutafuta na kushirikiana na wadau wa maendeleo wanaoweza kuunga mkono shughuli za afya katika maeneo wanayohudumu, hatua ambayo amesema itasaidia kupanua wigo wa huduma na kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Dkt. Lebba amewataka pia wataalamu hao kutumia ipasavyo mpangokazi utakaowekwa baada ya kikao hicho, akisisitiza kuwa utekelezaji wa mikakati hiyo unapaswa kuleta matokeo yanayoonekana katika utambuzi, matibabu na ufuatiliaji wa wagonjwa wa Kifua Kikuu na Ukoma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *