DKT. FATMA ATAKA USIMAMIZI MIKOPO YA ASILIMIA 10 SINGIDA UBORESHWE

Na Saulo Stephen – Singida.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga, amewataka wataalamu wa Halmashauri mkoani humo kuboresha namna ya kusimamia mikopo ya asilimia 10 kwa kutoa elimu, usimamizi na ufuatiliaji wa karibu kwa wanufaika, ili mitaji hiyo izalishe kipato, ichochee shughuli za kiuchumi na kusaidia wananchi kufikia kipato cha shilingi milioni 18 hadi 20 kwa mwaka.

Dkt. Mganga ametoa maelekezo hayo wakati akifungua kikao cha tathmini ya utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kilichofanyika katika Ukumbi wa Maktaba wa RC Mission, akisisitiza kuwa utoaji wa mikopo pekee hautoshi bila kuwawezesha wanufaika kuelewa namna ya kuendesha na kukuza biashara zao.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga.

Amesema mikopo hiyo inapaswa kutafsiri kwa vitendo malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuwaelekeza wanufaika shughuli zinazoweza kuwapatia kipato cha shilingi milioni 18 hadi 20 kwa mwaka.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa wanufaika kutenganisha mtaji na matumizi binafsi, kutunza kumbukumbu za fedha na kuwa na mipango ya biashara ili kuhakikisha mikopo hiyo inaleta matokeo yaliyokusudiwa.

Dkt. Mganga amesema Mkoa wa Singida umewezesha vikundi 518 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia Halmashauri saba kwa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 4.9, huku akizitaka Halmashauri kuongeza kasi ya utoaji wa mikopo na kuhakikisha matumizi yake yanafuatiliwa kwa karibu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Makatibu Tawala wa Halmashauri za Mkoa wa Singida ambaye pia ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Ikungi, Bw. Rashid Mohamed, amesema kikao hicho ni fursa ya kujitathmini, kubaini changamoto na kubadilishana uzoefu ili kuboresha utoaji na usimamizi wa mikopo hiyo.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Singida, Bw. Patrick Kasango, amesema kikao hicho kinalenga kuimarisha usimamizi wa uwezeshaji kiuchumi na kufuatilia namna mikopo hiyo inavyobadilisha maisha ya walengwa.

Wajumbe walioshiriki kikao hicho wameahidi kuongeza kasi ya utoaji wa mikopo, utoaji wa elimu na ufuatiliaji kwa walengwa, ili mikopo hiyo izalishe kipato, ajira na uchumi endelevu sambamba na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Mwenyekiti wa Makatibu Tawala wa Halmashauri za Mkoa wa Singida ambaye pia ni Katibu Tawala Wilaya ya Ikungi, Rashid Mohamed.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *