Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametoa katazo kwa kampuni zinazosimamia na kutekeleza miradi ya umeme nchini, kutonunua nje ya nchi vifaa vya umeme ambavyo vinazalishwa hapa nchini ili kukuza viwanda vya ndani vinavyozalisha vifaa hivyo, kuvipa thamani, kukuza ajira na uchumi wa nchi.
Dkt. Biteko ametoa agizo hilo Leo Novemba 15, 2023 Mkoani Mtwara wakati alipokagua miradi ya umeme vijijini na kuwasha umeme katika Kata ya Naliendele, eneo la Pachota A na Kijiji cha Nachenjele.
“TANESCO na REA, tabia ya kununua vifaa vya umeme nje ya nchi hiyo ni zilipendwa, viwanda vipo ndani ya nchi halafu vifaa vinanunuliwa nje, hivi vifaa vyetu mnataka tukauze wapi, kuanzia leo na kuanzia nilivyoingia ndani ya Ofisi lazima bidhaa zinazozalishwa hapa zinunuliwe na vifaa visivyopatikana ndani ya nchi ndio viagizwe kutoka nje, tukuze viwanda vyetu, tuvipe thamani na kukuza ajira.” Amesema Dkt. Biteko Aidha,
Dkt. Biteko amewataka wakandarasi wa umeme vijijini kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi na kueleza kuwa Serikali itafanya tathmini ya kila mkandarasi kuona alivyotekeleza miradi na ambao hawafanyi vizuri watasitishiwa mikataba kwani Serikali inalipa wakandarasi hao na itaendelea kuwalipa hivyo hawana sababu za kukwamisha Miradi ya Upelekaji Umeme Vijijini.
03:37 PM
Jack JAMBO FMadmin