DKT. BITEKO AMPONGEZA MWANAFUNZI ALIYE ELEZEA MIRADI YA UMEME

Na Josephine Maxime- Dar es Salaam.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ameagiza Mwanafunzi Mirabelle Msukari na Wenzake wa Shule ya Msingi Sun Rise iliyopo Wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam kupelekwa katika Mradi wa kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) ili kujifunza zaidi kwa Vitendo namna mradi huo unavyozalisha Umeme.

Dkt. Biteko amesema hayo kwa njia ya simu baada ya Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga kutembelea shule hiyo kwa lengo la kumpongeza mwanafunzi huyo ambaye video yake ilijizolea umaarufu kupitia mitandao ya kijamii ambapo Mirabelle alielezea kwa ufanisi juu ya miradi mbalimbali ya umeme inayotekelezwa nchini ukiwemo mradi wa Julius Nyerere.

‘’Sisi tukupongeze na tumefurahi kwa umri wako unafuatilia masuala ya Nishati, sasa tutakupeleka kuliona Bwawa la Julius Nyerere uone Umeme unavyozalishwa ili uendelee kujifunza zaidi. Sisi tunatamani kukuona ukifanikiwa zaidi,” amesema Biteko.

Kwa Upande wake Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema Miradi hii ya kimkakati ambayo inatekelezwa nchini ni jitihada za Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dokta Samia Suluhu Hassan ambaye ameonesha dhamira ya dhati kuendeleza miradi ya umeme nchini ukiwemo mradi wa JNHPP ambao kwa sasa umefikia asilimia 99.8.

“Wakati Mheshimiwa Rais anaingia madarakani, Mradi wa Julius Nyerere ulikuwa asilimia 33, leo tunavyozungumza umefikia zaidi ya asilimia 99 na mashine nane tayari zimeingizwa kwenye gridi ya Taifa. Imebaki mashine moja pekee ambapo mradi uko mbioni kukamilika,” amesisitiza mheshimiwa Kapinga

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa wateja, Irene Gowelle akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) , amesema wamepokea kwa vitendo agizo la Dkt. Biteko la kuhakikisha mwanafunzi huyo anafanya ziara katika Mradi wa Julius Nyerere ambapo pia amefafanua kuwa elimu na taarifa zinazotolewa na TANESCO zinawafikia walengwa kwa usahihi.

“Hatua hii inatupa nafasi ya kuona kwamba elimu na taarifa mbalimbali tunazozitoa zinawafikia moja kwa moja makundi mbalimbali i?wakiwemo watoto na ndio maana mmeweza kuona Mirabelle akizungumza kwa ufasaha.
Sisi kama Shirika la Umeme tutaendelea kufanya hivyo,” amefafanua Gowele.

Mwanafunzi huyo, licha ya pongezi pia amepewa zawadi mbalimbali ikiwemo Kompyuta Mpakato (Laptop) pamoja na fedha kiasi cha Shilingi Milioni Mbili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *