Na Gideon Gregory, Dodoma.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko amekemea vikali watu wanaohujumu miundombinu ya umeme ambapo amesema kuwa wanarudisha nyuma uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika kuwafikishia wananchi nishati ya uhakika na kuagiza Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuchukua hatua kali dhidi yao.
Dkt. Biteko ameyasema hayo Disemba 11,2024 Jijini Dodoma mara baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa kusafirisha umeme wa msongo wa taifa wa kilovoti 400 Chalinze – Dodoma na upanuzi wa vituo vya kupozea umeme vya chalinze vyenye kilovoti 400/220/132 na 400/220/33.
“Jambo hili tukilifumbia macho tukajenga miundombinu hii, ukija pale ukakata transfoma na mfumo wetu wa gridi ulivyo umejilinda maana yake ni kwamba utatoa mfumo wa laini nzima ya watu kupata umeme na wenzetu wa Tanesco hawalali usiku kucha wanafanya kazi lakini unakuta lipo kundi la watu wachache wanaorudisha nyuma jitihada za Serikali za kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma ya umeme kwakweli hili hatutolifumbia macho na hatutosita kuwachukulia hatua watakao bainika, “amesema.

Aidha amemtaka Mkandarasi anayetekeleza mradi huo kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kwa kiwango kilichowekwa ili kukidhi kiwango cha fedha kilochotolewa kwa kodi za Watanzania.
Pia Dkt. Biteko ametumia hafla hiyo kuwakumbusha viongozi na wananchi kuhusu jitihada za Serikali katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia katika kutimiza lengo lake la 80% ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
“Serikali imetoa ruzuku kwa mitungi ya gesi zaidi ya 400,000 itakayouzwa kwa nusu gharama ya bei ya soko na mitungi hii inasambazwa katika Mikoa yote Tanzania Bara, hivyo basi nitoe wito kwa Watanzania wote tutumie nishati safi ya kupikia kwa kutumia majiko ya gesi na teknolojia mbalimbali kulingana na mazingira ikiwemo nishati ya umeme kwani nishati hizi ni miongoni mwa nishati safi, salama na ya gharama nafuu ikilinganishwa na matumizi ya kuni na mkaa,”amesema.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Innocent Bashungwa amesema watahakikisha miundombinu ya mradi huo inakuwa salama huku akiwaonya watakaoharibu miundombinu kuwa watapambana nao.
“Serikali inatoa fedha nyingi ili kutekeleza miundombinu hii ya umeme hivyo Wizara yangu itahakikisha miundombinu yote hii inalindwa kwa wivu mkubwa na kuwashughulikia wahalifu wote watakaojitokeza kuiharibu,”amesema.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga amesema mradi huo umegawanyika katika sehemu kuu mbili ambazo ni ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme katika msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma yenye urefu wa kilomita 345 na upanuzi wa vituo vya kupokea na kupoza Umeme vya Chalinze (400/220/132kV) mkoani Pwani na Zuzu (400/220/33kV) Mkoani Dodoma.
Pia ameelezea kuwa malengo ya mradi huo ni kuwezesha usafirishaji wa umeme wote (2,115MW) utakaozalishwa katika Bwawa la JNHPP na kuufikisha kwenye maeneo yote ya mahitaji ya umeme, hatua itakayosaidia kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme kwenye Gridi ya Taifa na kuongeza uwezo wa kusafirisha umeme kwenda mikoa yenye viwanda na migodi ya uchimbaji madini ya Kaskazini Magharibi, Kaskazini Mashariki, Kanda ya Kati na Kusini mwa Tanzania.

“Lengo lingine la mradi huu ni kuwezesha zoezi la uunganishaji umeme kwa pamoja katika mifumo ya Mashariki mwa Afrika (Eastern Africa Power Pool – EAPP) na Kusini mwa Afrika (Southern Africa Power Pool – SAPP) na hivyo kuwezesha kufanyika kwa biashara ya nishati ya umeme kikanda (Regional Power Trading),”amesema.
Amesema Mradi husika unagharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100 kwa jumla ya gharama ya Shilingi 513 Bilioni ambapo Mkandarasi Kampuni ya TBEA kutoka China ameshalipwa malipo ya awali ya kiasi cha Shilingi bilioni 107.93 ambayo ni asilimia 20 ya gharama za mradi.