Mahakama ya Wilaya ya Uvinza Mkoa wa Kigoma imemuhukumu mshitakiwa Ruben Gerishon(24),Dereva pikipiki,mkazi wa Kijiji cha Mlela wilayani Uvinza kwenda jela miaka 30 na kutaifisha Pikipiki yenye namba za usajili MC 601 DLB aina Kinglion mali ya mtuhumiwa kuwa mali ya Serikali baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumbaka binti mmoja (24).
Mshitakiwa alitenda kosa hilo Septemba 07,2023 huko Kijiji cha Mlela Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma baada ya kukodiwa kumpeleka muhanga kutoka kijiji cha kidawe Wilaya ya kigoma kwenda kijiji cha Mlela wilayani Uvinza na kutekeleza uhalifu huo wakiwa njiani.
Akitoa hukumu hiyo hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Uvinza Misana Majura amesema kuwa Mahakama imejiridhisha pasipo na shaka ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka na hatimaye kumtia hatiani mshitakiwa kwa kosa hilo.
Mshitakiwa huyo amehukumiwa kifungo hicho ili iwe fundisho kwa wahalifu wanao jihusisha na vitendo vya ukiukaji wa sheria,maadili na ukatili dhidi ya wanawake.