
Na Gideon Gregory,Dodoma
Hadi Machi 2024, deni la Serikali lilikuwa shilingi Trilioni 91.7 ikilinganishwa na shilingi Trilioni 77 katika kipindi kama hicho mwaka 2023, sawa na ongezeko la asilimia 19.1.
Hayo yameelezwa leo Juni 13,2024 Bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo wakati akiwasilisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2024/25 kuelekea kusomwa kwa bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha.
“Ongezeko la deni limechangiwa na kupanda kwa viwango vya kubadilisha fedha pamoja na kuongezeka kwa riba kwenye mikopo ya nje ambayo riba zake hutegemea mabadiliko ya hali ya soko (floating rates)”, amesema.
Aidha, amesema kati ya kiasi hicho, deni la ndani lilikuwa shilingi Trilioni 30.7 na deni la nje lilikuwa shilingi Trilioni 60.9 na kwamba ongezeko la deni lilitokana na Serikali kuendelea kupokea fedha za mikopo ya zamani na mipya kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, viwanja vya ndege, umeme na maji.
Waziri wa Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo amesema thamani ya shilingi ya Tanzania imeshuka kwa 3.5% mwaka 2023 ikilinganishwa na 0.2% mwaka 2022.
Prof. Mkumbo ameyabainisha hayo leo Juni 13,2024 Bungeni Jijini Dodoma wakati akiwasilisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2024/25 kuelekea kusomwa kwa bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha huku akiongeza kuwa kupungua kwa thamani ya shilingi kulichangiwa na hatua zilizochukuliwa na nchi zilizoendelea katika kukabiliana na mfumuko wa bei ikiwemo utekelezaji wa sera ya fedha yenye lengo la kupunguza ujazi wa fedha.
“Utekelezaji wa sera hiyo ulisababisha kupanda kwa viwango vya riba ya dola ya Marekani kutoka asilimia 3.78 Novemba 2022 hadi asilimia 5.5 Agosti 2023 na hivyo, kuvutia uwekezaji katika masoko ya fedha ya Marekani na kusababisha upungufu wa dola katika mataifa mengine”,amesema.
Poa amesema katika kuimarisha utulivu wa shilingi, Benki Kuu ya Tanzania ilichukua hatua mbalimbali zilizowezesha kuongeza fedha za kigeni katika soko la fedha za kigeni, ikiwemo kuuza dola pamoja na kutekeleza sera ya fedha yenye lengo la kupunguza ukwasi wa shilingi.
“Aidha, Serikali ilianzisha mkakakti wa kuimarisha sekta za uzalishaji na huduma ikiwemo kilimo, uvuvi, samaki, utalii, madini na nishati mwaka 2023 kwa lengo la kuongeza mauzo nje na mapato ya fedha za kigeni” amesema.