Na Pascal Tuliano, Tabora.
Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Upendo Wella, ametoa wito kwa wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 kutoka Halmashauri kurejesha kwa wakati, ili kuwanufaisha wengine wenye uhitaji.
DC Wella ametoa kauli hiyo wakati akizungumza katika viwanja vya makao makuu ya Manispaa ya Tabora, wakati wa hafla ya utoaji hundi za mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 187 kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

Mikopo hiyo, ambayo imetolewa kwa vikundi nane kupitia mpango wa asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, inalenga kuwainua kiuchumi wananchi hao bila riba, ambapo DC Wella aliwataka wanufaika kurejesha mikopo kwa wakati ili kuhakikisha fursa hizo zinaendelea kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya pia amekabidhi pikipiki sita kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii, zikiwa na lengo la kurahisisha huduma kwa wananchi akiwataka maafisa hao kuzitumia pikipiki hizo kwa maslahi ya umma na kuhakikisha zinasaidia katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Dkt. John Pima, amesema mikopo ya asilimia 10 isiyo na riba imekuwa msaada mkubwa kwa vijana katika kujikwamua na umaskini huku akitoa mfano wa vikundi kutoka kata za Ntalikwa na Itonjanda ambavyo tayari vimepiga hatua kubwa kiuchumi kupitia mikopo hiyo.
Aidha, viongozi hao wameishukuru serikali kwa kuendelea kuruhusu mpango huo wa mikopo bila riba kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, wakisisitiza kuwa matokeo chanya ya mikopo hiyo yanaanza kuonekana kwa muda mfupi.


