Katika kutekeleza maagizo ya Serikali ya kuhakikisha wanafunzi wanapata huduma ya maji safi na salama shuleni na kuondokana na changamoto ya kubeba madumu ya maji, wadau wa ufadhili wanaotambulika kwa jina la Viva Con Agua, wameendelea kuunga mkono jitihada hizo kwa kutekeleza miradi ya maji, usafi na mazingira katika shule mbalimbali.
Viva Con Agua, wamewezesha kusogeza huduma ya maji hadi maeneo ya shule kwa kuunganisha maji kutoka kwenye visima au chemichemi, pamoja na kuweka matanki ya kuhifadhia maji shuleni.
Aidha, wamejenga matundu ya vyoo kwa lengo la kuboresha huduma za usafi na mazingira kwa wanafunzi.

Hatua hiyo, imekuja katika kuunga mkono agizo la Serikali kwamba kuanzia mwaka wa fedha 2026/2027, watoto hawapaswi kuendelea kubeba madumu ya maji kwenda shuleni na kusiwepo na changamoto ya upungufu wa matundu ya vyoo katika shule.
Akizungumza Septemba 2, 2026, alipotembelea katika shule tatu ambazo miradi hiyo imetekelezwa kwa ufadhili wa Viva Con Agua, Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Michael Semindu, amewashukuru na kuwapongeza kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha huduma za kijamii, hususan maji, usafi na mazingira.

Semindu amesema, ushirikiano kati ya Serikali na wadau mbalimbali ni muhimu katika kutekeleza maagizo ya Serikali na kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora, salama ya kujifunzia.
Aidha, amewataka walimu, wanafunzi na wananchi kuhakikisha wanatunza miundombinu ya maji na usafi iliyowekwa, ili iweze kudumu na kuendelea kutoa huduma kwa muda mrefu.

“Utunzaji wa miundombinu hiyo ni jukumu la pamoja, hivyo kila mmoja anapaswa kuitumia kwa usahihi, kuilinda dhidi ya uharibifu na kutoa taarifa mapema pale changamoto zinapojitokeza,” amesisitiza Semindu.
Kwa upande wao, Walimu na Wanafunzi wamesema, kuimarishwa kwa huduma ya maji na usafi shuleni kutasaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia, kuongeza usafi na kupunguza changamoto ya wanafunzi kutumia muda wao kutafuta maji.

Aidha, wameahidi kushirikiana katika kuhakikisha miundombinu hiyo inatunzwa na kutumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa, ili iweze kunufaisha wanafunzi na jamii kwa ujumla kwa muda mrefu.
Hatua ya Viva Con Agua, inaendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na wadau katika kuboresha huduma za maji, usafi na mazingira, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha wanasoma katika mazingira bora na salama.



