Na Saulo Stephen – Singida.
Serikali Wilayani Singida, imeagiza kukamilika kwa wakati miradi ya elimu yenye thamani ya takribani milioni 600, ikiwemo madarasa na Matunda ya Vyoo mpaka kufikia Desemba 10 Mwaka huu iwe imekamilika, ili Wanafunzi watakaonza shule mwezi januari mwakani wakute miradi hiyo ipo tayari.
Maagizo hayo yametolewa na Mkuu wa Wilaya ya Singida, Godwin Gondwe kuhusu Miradi ya Elimu inayotekelezwa chini ya mpango wa BOOST, ambapo akiwa katika ziara yake ya kutembelea shule za msingi Uhamaka, Kimai, Unyankhae, Mwaja na Unyamikumbi B, Dc Gondwe amesisitiza kuhusu umuhimu wa kusimamia kikamilifu na kwa ubora miradi hiyo, ili kufikia Malengo ya Serikali.

Aidha, ameongeza kuwa miradi hiyo ni sehemu ya juhudi za serikali kuboresha miundombinu ya elimu katika Manispaa ya Singida ili wanafunzi waendelee kupata elimu katika mazingira yaliyo bora na salama.
Katika hatua nyingine DC Gondwe amewataka Walimu katika wilaya ya Singida kuendelea kuhakikisha chakula kinapatikana shuleni na wanafunzi wanakula kwa asilimia 100 ilikuendelea kuongeza ufaulu mashuleni.