Na Daniel Gahu – Katavi.
Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Katavi limepokea gari ambalo litarahisisha utekelezaji wa majukumu ya shirika hilo ndani ya wilaya ya Tanganyika, ambapo gari hilo limekabidhiwa na Mkuu wa wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu huku akiagiza matumizi sahihi ya gari hilo.
Amesema hayo wakati wa makabidhiano ya Gari hilo aina ya crane, litakalotumika kubebea nguzo za zege na kuzisambaza katika maeneo mbalimbali ndani ya Wilaya hiyo ya Tanganyika huku akipiga marufuku matumizi ya pombe wakati wa uendeshaji wa gari hilo.

“Chombo hiki sio cha kuendesha huku umekunywa pombe, chombo hiki sio cha kuendesha huku umelewa pombe, chombo hiki ni cha kuendesha huku ukiwa na akili zako timamu”,
“Sasa kama utaona umeenda kumwagilia moyo basi hiyo siku usiendeshe gari, bora utafute mtu mwingine aiendeshe. Na kama atakosekana kabisa wakuiendesha basi mniite mimi mwenyewe niiendeshe” amesema DC Buswelu.

Amebainisha kuwa ufanisi katika utendaji kazi wa Shirika la TANESCO wiliya ya Mpanda unazidi kuongezeka Kwasababu ya kuongezewa vitendea kazi hivyo haina sababu ya msingi kuona wananchi wakilalamikia huduma kutoka katika shirika ambalo limepatiwa uwezeshaji na Serikali wa vifaa bora na kisasa.
Ameongeza kwa kazi zote zote zile za Serikali ambazo zitahitaji usaidizi wa hili gari (Crane) litoe usaidizi wa haraka na lifanye kazi kwaajili ya maslahi mapana ya wananchi wa Tanganyika.
“Pindi yanapotea maafa naomba gari hili pia liwe sehemu ya uokozi kwa kushirikiana na mashirika mengine ya Umma,” amesema DC Buswelu.

Pia, ametoa maelekezo kwa shirika hilo kumsimamia mkandarasi wa huduma ya umeme vijijini REA kufanya kazi usiku na mchana ili vijiji vyote vilivyopo ndani ya halmashauri ya wilaya ya Tanganyika vipate huduma ya umeme.
“Juzi nilikuwa Kijiji cha Ifinsi, wananchi wamelalamika kutokupata huduma ya umeme licha ya kuwa wameshakamilisha taratibu zote za kupatiwa huduma ya umeme, tunataka kuona Kila alipo mwananchi basi na huduma ya umeme iwe imefika,” amesema DC Buswelu.

Aidha, kwa upande wake kaimu Meneja mkuu wa shirika la umeme wilaya ya Tanganyika TANESCO, Adam Ally ameishukuru Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwapatia gari hilo kwani litarahisisha utendaji kazi wa Shirika hasa kubebea nguzo nzito za zege huku akitoa ahadi ya kulitunza gari hilo ili liweze kudumu kwa muda mrefu.
“Nina amini nguzo zote za zege tutazibeba kwa urahisi na kwa wakati jambo ambalo litasaidia kutoa huduma kwa wakati kwa wananchi wote wa Tanganyika,” amesema Meneja Adam.

Naye Injinia Yoram Gaitan Mtemi, Kaimu Meneja wa TANESCO Mkoa wa Katavi amesema gari hiyo waliyopewa kwa awamu ya pili litakuwa chachu ya kutatua changamoto za wananchi hasa wa wilaya ya Tanganyika ambapo hapo awali kulikuwa na changamoto ya kukatika katika kwa umeme kutokana na kushindwa kufika katika maeneo yenye changamoto kwa wakati.
Hivyo usafiri huo utaliwezesha shirika la umeme wilaya ya Tanganyika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwa wakati huku akibainisha kwa sasa wanakwenda kutumia nguzo za zege ambazo hapo awali katika wilaya hiyo zilishindwa kutumika kutokana na kukosa gari ya crane yenye uwezo wa kuzibeba nguzo hizo.


