DC APSON AWATAKA WATENDAJI IKUNGI KUTEKELEZA KWA UFANISI MKATABA WA LISHE

Na Saulo Stephen – Singida.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Thomas Apson, ameongoza Kikao cha Kawaida cha Tathmini ya Mkataba wa Lishe na Jiongeze Tuwavushe Salama cha Wilaya, kilichowakutanisha wadau na watendaji mbalimbali kwa lengo la kutathmini utekelezaji wa mkataba huo na kuweka mikakati ya kuimarisha hali ya lishe kwa wananchi.

Akizungumza katika kikao hicho, Apson amewataka watendaji wote kusimamia kikamilifu majukumu yao na kuhakikisha wanatekeleza kwa ufanisi wajibu unaohusiana na utekelezaji wa Mkataba wa Lishe na Jiongeze Tuwavushe Salama.

Amesema mafanikio ya mkataba huo yanategemea ushirikiano, uwajibikaji na utekelezaji wa vitendo, huku akisisitiza kuwa maazimio yanayofikiwa kwenye vikao hayapaswi kubaki kwenye maandishi, bali yageuzwe kuwa hatua zinazotoa matokeo kwa wananchi.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Bi. Haika Massawe, amewapongeza watendaji na wadau kwa juhudi wanazoendelea kuzifanya katika kutekeleza majukumu yao.

Amewataka kuendelea kufanya kazi kwa moyo wa kujituma, uwajibikaji na ushirikiano ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa na huduma zinazolenga kuboresha hali ya lishe kwa wananchi zinaendelea kutolewa kwa ufanisi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *