Daktari adaiwa kulewa hivyo akasababisha mjamzito kufariki

Wananchi wa kata ya Ngarenairobi, iliyopo wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro wamevamia kituo cha afya cha Ngarenairobi, kinachomilikiwa na kanisa katoliki wilayani humo wakituhumu mmoja wa madaktari aliyemfanyia upasuaji mama mjamzito alikuwa amelewa na kusababisha kifo chake.

Dainess Thomas Massawe(35) alifariki usiku wa Septemba 20, mwaka huu baada ya kupelekwa katika kituo hicho cha afya kwa ajili ya kujifungua.

Inadaiwa kuwa baada ya mwanamke huyo kushikwa na uchungu akiwa nyumbani kwakwe na kuwahishwa katika kituo hicho cha afya saa nne usiku alipofika kituoni hapo hakupata huduma kwa muda huo mpaka alipopata huduma saa nane usiku baada ya wagonjwa waliokuwepo wodini kupiga ukunga kuomba msaada wa madaktari kutokana na uchungu aliokuwa nao ambapo kwa wakati huo walikuwa hawapo.

Elikunda Ikera ambaye ni mume wa marehemu amesema mke wake alipofikishwa hospitalini hapo akiwa na uchungu alishindwa kupata huduma kwa wakati licha ya wagonjwa waliokuwepo wodini kupiga ukunga kuita madaktari lakini hawakupatikana kwa wakati.

“Na wakati huu tulifika hospitali saa nne usiku lakini daktari alikuja saa saba usiku akiwa amelewa, walimchukua mke wangu na kumpeleka chumba cha upasuaji, walimfanyia upasuaji wakamtoa mtoto na kisha akarejeshwa wodini, wakawa wamemtundikia dripu ya damu, ilipofika saa tatu na nusu asubuhi yule mama alifariki,”

Kufuatia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Siha, Christopher Timbuka, amesema imepelekwa timu ya wataalam kutoka mkoani na wilayani humo kwenda katika kituo hicho cha afya kuchunguza na kuangalia kifo cha mama huyo kilisababishwa na nini ili ziweze kuchukuliwa hatua kwa wahusika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *