Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kimetoa msaada wa vitu mbalimbali vikiwemo sabuni, dawa za meno, maziwa, taulo za watoto (pampasi) na mahitaji mengine kwa wagonjwa, hususani akinamama waliojifungua na wanaotarajia kujifungua katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou-Toure.
Akizungumza wakati wa kutoa msaada huo, Rais wa CWT, Suleiman Ikomba, amesema kuwa lengo la zoezi hilo ni kutoa huduma kwa jamii kama sehemu ya ibada na kurudisha fadhila kwa jamii inayowazunguka.

“Tumekuja hapa kuonesha kwamba chama cha walimu sio tu kinashughulika na mambo ya walimu, bali pia kinaunga mkono jamii kwa ujumla. Ni furaha yetu kuona kwamba kwa namna yoyote tunaweza kuishika jamii kwa mtindo huu,” alisema Ikomba.
Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Rasilimali Watu na Utawala Mkoa wa Mwanza, Daniel Machunda ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa, alisema serikali ya mkoa inaendelea kushirikiana kwa karibu na CWT katika shughuli za kijamii ikiwemo kuimarisha sekta ya elimu na afya.

“Tunaishukuru CWT kwa msaada huu na tunawatakia ukaribu zaidi katika shughuli zao za kijamii na vikao vya baraza vya chama mkoani hapa,” alisema Machunda.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Dkt. Bahati Msaki, alisema msaada huo umekuja kwa wakati muafaka, hasa kwa akinamama wanaojifungua, na aliwakaribisha wadau wengine kuja kutoa misaada kwa wagonjwa.

“Tunaishukuru CWT kwa faraja waliyoileta kwa wagonjwa na tunawakaribisha tena kwa nyakati nyingine,” alisema Dkt. Msaki.
Baadhi ya wagonjwa waliopokea msaada huo waliwashukuru CWT kwa kuwapatia vifaa kama pampasi, maji na nepi za watoto, na kueleza kuwa msaada huo utasaidia katika kuwahudumia watoto wao na kuonyesha kuwa wanathaminiwa.

Chama cha Walimu Tanzania kimesisitiza kuwa kinashirikiana na serikali katika kuunga mkono sekta ya elimu na afya kwa kujenga na kuboresha miundombinu ya madarasa na vituo vya kutolea huduma za afya, na hivyo kutoa mfano wa mshikamano kati ya wadau wa kijamii na jamii kwa ujumla.



