Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Mgombea Uraisi kupitia Chama cha wananchi (CUF) Gombo Samandito Gombo amewahaidi Wananchi wa mkoa wa Shinyanga neema endapo atafanikiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ni pamoja na kufuta gharama za matibabu na kutoa elimu bure kuanzia chekechea hadi chuo kikuu.
Gombo amezungumza hayo katika mkutano wa kampeni wa kuomba ridhaa ya wananchi ili kukichagua chama hicho katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, uliofanyika katika katika uwanja wa stand ya zamani uliopo katika manispaa ya Shinyanga huku akianisha kuwa mapato yatokanayo madini kilimo na ufugaji yatagharimia mahitaji hayo.

“Mkinichagua mimi nitafuta gharama za matibabu, na elimu itakuwa bure kuanzia chekechekea hadi chuo kikuu,” amesema Gombo.
Kwa upande wa watumishi wa umma, Gombo amesema endapo watafanikiwa kuingia madarakani watakwenda kufuta utaratibu wa vikokotoo kwa wastaafu ikiwa ni pamoja na kuondoa mikopo kwa majeshi na watumishi wote wa umma wanaodaiwa na mabenki.

Awali, akizungumza na hadhara hiyo, Mgombea mwenza wa nafasi ya uraisi wa chama hicho, Husna Mohammed Abdallah amewaomba wananchiwa wa mkoa huo kukichagua chama cha wananchi CUF, huku akielezea utajiri wa madini uliopo mkoani Shinyanga akihusianisha na masiha halisi ya wananchi wa mkoa huo.
Amesema mkoa huo unazalisha madini ya almasi ambayo ndiyo madini ghali Zaidi duniani katika soko la dunia na kwamba kareti moja ya almasi inauzwa kwa dola 4000 ambayo ni sawa na shilingi miliono kumi za kitanzania hivyo garamu moja ya almasi haipungui jumala ya shilingi milioni 40 za kitanzania hivyo mkoa huo ulipaswa kuwa na maendelo ya miundombinu yenye kutosheleza.

“Wakati nafika Shinyanga nilishangaa nikajiuliza hapa ndiyo kwenye utajiri wa madini kweli mbona hapana uwiano na madini yanayozalishwa,” amesema Husna.
Naye mgombea ubunge wa jimbo la Shinyanga Mjini, Mshandete Gerald ameomba ridhaa ya wananchi wa jimbo hilo kumchagua, huku akiaInisha baadhi ya miradi ya maendeleo atakayokwenda kuitekeleza endapo ataingia madarakani ikiwemo uimarishaji wa huduma katika hospital ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga pamoja na kukamilisha kipande cha barabara ya nguzo nane Mwawaza kwa kiwango cha lami.


