COPRA WATOA TANI 50 ZA MBEGU YA ALIZETI MKOANI GEITA

Na Frank Aman – Geita.

Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), imetoa jumla ya tani 50 za mbegu ya alizeti mkoani Geita kama sehemu ya kusaidia wananchi kujikwamua kiuchumi kupitia sekta ya kilimo.

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa COPRA, Sezaria Makota alikabidhi mbegu hizo mbele ya mkuu wa mkoa wa Geita na kueleza mbegu hizo za alizeti zitagawiwa katika wilaya zote za mkoani humo.

Amesema mbali na kugawa mbegu za alizeti kwa wakulima wa Geita, COPRA pia imejipanga kuwaletea kwa ajili ya uhakika wa soko, na mnunuzi huyo ataingia mkataba na wakulima waliogawiwa mbegu.

“Sisi kama Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mcahanganyiko tunachowaahidi, tutaacha ofisa wetu mmoja hapa katika mkoa wa Geita na nimefuatana naye, ambaye atakuwepo hapa muda wote.

“Lengo la Mamlaka ni  kuhakikisha hatua zote kuanzia upandaji kwa nafasi, upandaji kwa kuzingatia muda hadi mauzo ya alizeti hii kwa nafasi yetu kama COPRA tutahusika”, amesema Sezaria.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mohamed Gombat amesema mbegu za alizeti zilizotolewa zitatosha katika takribani hekari 25,000 na matarajio yakiwa ni kuzalisha kati ya tani 20,000 hadi 30,000.

“Mbegu hii itakuwa msaada zaidi kwa sababu katika mkoa wa Geita, kwani tuna viwanda vikubwa na vya kati vya kuzalisha mafuta ya alizeti visivyopungua 31 katika halmashauri zetu sita, amesema Gombati.

Mkuu wa mkoa wa Geita, Martine Shigella amesema mbegu hizo zimezalishwa nchini, zimepitia taratibu zote, zimethibitishwa na watalaamu wa ndani na zina uwezo wa kukomaa ndani ya miezi miwili mpaka miezi mitatu.

“Mbegu hizi hazina tishio kwa sababu zimezalishwa ndani ya nchi yetu na watalaamu wetu na zimepita kwenye taratibu na kanuni ambazo watalaamu wetu wa kilimo wameweza kuthibitisha kwamba zinafaa”, amesema.

Shigella amewataka wakuu wa wilaya wote kusimamia zoezi la ugawaji wa mbegu hizo za alizeti ziweze kuwafikia wakulima ambao ni walengwa ndani ya wiki moja bila kikwazo cha aina yeyote.

“Ni imani yangu tunaenda kubadilisha sura ya uchumi wa wananchi wetu, si tu kwa kutegemea uzalishaji wa madini ya dhahabu, lakini vilevile wakulima waamini serikali inafanya jitihada kuwawezesha.

“Tukajipange vizuri, tukawagawie wakulima wetu, tukawape elimu, namna ya upandaji, tuwafuatilie, tuwasimamie, ili matokeo ya kazi tunayoifanya leo tuje tuione mwezi wa sita, mwezi wa saba”, amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *