CHIEF MGONTO AHAMASISHA MICHEZO AKITOA MIPIRA KWA TIMU ZA IKUNGI

Na Saulo Stephen, Ikungi – Singida.

Mbunge wa Jimbo la Ikungi Mashariki, Chief Thomas Mgonto, ameendelea kuonesha dhamira ya kuendeleza michezo kwa kushiriki shughuli mbalimbali za michezo katika Kata ya Ikungi, akisisitiza kuwa michezo ni nyenzo muhimu ya kujenga afya, umoja na kuibua vipaji kwa vijana.

Katika ziara hiyo, Mgonto alitembelea Klabu ya Draft ya Ikungi Mjini ambapo alishiriki mchezo wa draft pamoja na wanachama wa klabu hiyo, akizungumza nao kuhusu umuhimu wa michezo katika kuimarisha mshikamano wa jamii.

Mbunge huyo pia alijumuika na vijana wa Kata ya Ikungi kucheza mchezo wa pool table, huku akiwapongeza kwa kutumia michezo kama njia ya kujenga urafiki, nidhamu na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha maisha yao.

Aidha, Mgonto alikabidhi mipira kwa timu mbalimbali za Kata ya Ikungi ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono maendeleo ya soka katika eneo hilo. Aliahidi kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha Wilaya ya Ikungi inapata Chama cha Soka kitakachosaidia kuratibu mashindano, kukuza vipaji na kuinua kiwango cha mchezo huo.

Akizungumza na wananchi na vijana waliojitokeza katika shughuli hiyo, Mgonto alisema ataendelea kuwekeza katika sekta ya michezo kwa kuwa ina mchango mkubwa katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi, huku akiwahimiza vijana kuitumia michezo kama fursa ya kujenga maisha yao na kuitangaza Ikungi kitaifa na kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *