Mwenyekiti wa Madiwani wa Chama cha ACT-Wazalendo, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kazuramimba Wilayani Uvinza Mkoani Kigoma, Musa Chesa, ameahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa wakati na kuwanufaisha wananchi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo, Agosti 14, 2026 mjini Kigoma, Chesa amesema atahakikisha anasimamia haki, ukweli na uwajibikaji katika nafasi yake ya udiwani na Mwenyekiti wa madiwani wa chama cha ACT – Wazalendo Tanzania, ili kila mwananchi apate haki yake na kunufaika na matokeo ya usimamizi bora wa miradi ya maendeleo.

Aidha amesema atatumia nafasi yake ya udiwani pamoja na uongozi wa madiwani wa ACT-Wazalendo kuhimiza ushirikiano, uwajibikaji na mawasiliano mazuri kati ya wananchi, Halmashauri na Serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Kata ya Kazuramimba miradi mbalimbali ya maendeleo imeendelea kutekelezwa kwa lengo la kusogeza huduma muhimu za kijamii karibu na wananchi na kuwaondolea adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma” Amesema Chesa.
Ameutaja ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kazuramimba kuwa miongoni mwa miradi hiyo, akisema kituo hicho kinatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni na kitasaidia kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wa kata hiyo na maeneo jirani.

Kwa upande wao, baadhi ya viongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo Mkoa wa Kigoma, akiwemo Mwenezi wa chama hicho, wamesema Mwenyekiti wa Madiwani wa ACT-Wazalendo Tanzania ana jukumu la kusimamia malengo ya chama kwa kuhakikisha anafika katika kata mbalimbali, kusikiliza changamoto za wananchi na kushirikiana nao katika kuzitafutia ufumbuzi.
Viongozi hao, wameeleza kuwa ushirikiano kati ya viongozi, wananchi, Halmashauri na Serikali ni muhimu katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi na inaleta matokeo yanayotarajiwa kwa jamii.


