
Mbunge wa jimbo la Ushetu Emmanuel Cherehani amewataka wakulima wa Tumbaku katika mkoa wa kitumbaku Kahama kuacha tabia ya kuchanganya madaraja ya Tumbaku wakati wa ufungaji wa mavuno ya zao hilo na kwamba Tumbaku yenye ubora inatafutwa shambani na siyo Sokoni.
Hayo ameyasema leo April 30,2024 katika uzinduzi wa soko la kwanza la Tumbaku lililofanywa na kampuni ya ununuzi wa Tumbaku ya Alliance One kwenye chama cha msingi Ngokolo kufuatia mmoja kati ya wakulima wa chama cha Msingi Ngokolo kuchanganya madaraja ya Tumbaku kwenye mitumba sita kati ya Ishirini na tano aliyoingiza sokoni.

Cherehani ameongeza kuwa lengo la Halmashauri ya Ushetu ni kuingia kwenye uzalishaji wa Kilo milioni thelathini za Tumbaku na kwamba serikali imefuta kodi na madeni mbalimbali kwa wanunuzi wa tumbaku ili kuvutia wawekezaji na kwamba kuwachanganyia tumbaku kwa madaraja yasiyolingana kunaweza kuwafanya wanunuzi kuondoka na kuacha kununua tumbaku Kahama.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama kikuu cha Ushirika KACU Tano Nsabi amemshukuru Cherehani kwa kuhudhuria Katika soko la ununuzi wa Tumbaku na kutoa wito kwa wakulima akiwataka kubadilika na kuzingatia ubora wa tumbaku na kuacha kuchanganya madaraja kama alivyoagiza Mbunge na kuwataka wateuzi na wanunuzi kuwatendea haki wakulima.
Naye mkulima Juma Charles aliyechanganya madaraja katika mitumba sita ya Tumbaku ameomba radhi kwa chama chake cha msingi na Mkoa wa Kitumbaku kwa ujumla na kuahidi kurudia kufunga mavuno yake kwa kufuata madaraja.



