
Na Adam Msafiri, Mara.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Mara Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Pius Lutumo leo hii akiongea na waandishi wa habari mkoani humo,amethibitisha kutokea kwa ajali ya gari iliyosababisha kifo cha Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la umeme Tanzania(Tanesco) Mhandisi Gissima Nyamohanga pamoja na dereva wake usiku wa kuamkia leo wilayani Bunda mkoani Mara.

Kamanda Lutumo amesema ajali hiyo imetokea wakati dereva wa gari iliyokuwa imembeba Mkurugenzi huyo Mtendaji wa Tanesco,kushindwa kumudu gari wakati akijaribu kumkwepa mwemdesha baiskeli na kupelekea kugongana uso kwa uso na lori.
‘Usiku wa kuamkia leo kulitokea ajali ya magari mawili kugongana uso kwa uso kati ya gari dogo aina ya Toyota LandCruiser lenye namba za usajili T 385 EHM na lori aina ya Scania T396 EHR likiwa na tela lenye namba za usajili T833 ACD na kusababisha vifo vya watu wawili,ajali hiyo imetokea tarehe 13 Aprili 2025 majira ya saa 7 na nusu usiku huko Nyatwali-Ndabaka eneo la hifadhi ya Serengeti wilaya ya Bunda mkoani Mara katika barabara ya Mwanza-Musoma’ Amesema Kamanda Lutumo.

Aidha Kamanda Lutumo amebainisha kuwa”Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari dogo kumkwepa mwendesha baiskeli na kushindwa kulimudu gari lake na hivyo kugongana uso kwa uso na lori alilokuwa anapishana nalo,hata hivyo dereva wa lori alikimbia na kuelekea kusikojulikana mara baada ya ajali kutokea”.
Hata hivyo taarifa ya Polisi inaema kuwa miili ya marehemu hao wawili imehifadhiwa katika hospitali teule ya DDH wilaya ya Bunda,huku rai ikitolewa kwa madereva kuzingatia sheria wawapo barabarani ili kuepusha ajali zitokanazo na uzembe.


