Serikali imetoa onyo kwa watu wanaopotosha kuhususiana na chanjo ya ugonjwa wa kichocho na minyoo ya tumbo, huku agizo likitolewa kwa walimu wakuu katika Shule zote za Msingi za Manispaa ya Shinyanga kutoa chakula saa moja kabla ya chanjo hiyo itakayoanza kutolewa kuanzia Novemba 24, ili kuzuia maudhi madogo madogo yanayoweza kujitokeza.
Onyo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Johari Samizi wakati akizungumza na kamati ya afya ya msingi wilaya ya Shinyanga katika kikao elekezi kuhusiana na chanjo hiyo ambapo amesema zaidi ya watoto 45,000 katika Halmashauri Ya Manispaa ya Shinyanga watapata tiba kinga hiyo.
Kwa upanda wake Afisa Mipango kutoka Wizara ya Afya katika kitengo cha mpango wa Taifa wa kudhibiti magonjwa yasiyopewa kipaumbele Steven Mbwambo ameelezea malengo ya wizara hiyo katika kutoa kinga tiba kwa watoto hasa walioko mashuleni hususan kwenye mikoa sita iliyopo katika ukanda wa ziwa Victoria .
Magonjwa yasiyopewa kipaumbele yamekuwa yakipuuzwa na jamii ambapo serikali imeamua kuyadhibiti kwa kutoa chanjo kwa watoto kuanzia umri wa miaka 5 hadi 14 ikiwa ni utekelezaji wa azimio la nchi za Afrika zilizoketi Kigali nchini Rwanda tarehe 27 January 2o22 na kusainiwa na Rais Dkt.Samia Suluhu lengo likiwa ni kujitoa kwa asilimia 100% kuhakikisha tanzania inatokomeza magonjwa hayo ifikapo mwaka 2030.