Chama cha Viziwi Kahama Chaiomba Serikali Kuajiri Mkalimani

Chama Cha viziwi Tanzania (CHAVITA) Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga kimeiomba serikali kuajiri wakalimani watakaowasaidia kutafsiri lugha ya alama ili waweze kupokea na kuelewa ujumbe unatolewa katika mikutano na vikao mbalimbali pamoja na kutambua na kuzitumia fursa za kiuchumi

Wito huo umetolewa leo April,26,2024 na Baadhi ya wanachama wanaounda chama hicho wakati wakiongea na Jambo Fm Kwa lugha ya alama kwa msaada wa Mwenyekiti wa Chama hicho Manispaa ya Kahama Zawadi Masood ambaye amesema kuwa wilaya hiyo ina walemavu wengi wa kusikia wanaohitaji wakalimani na kwamba yeye binafsi mekuwa akijitolea kuwasaidia wenzake pale inapobidi na kuiomba Manispaa kuajiri mkalimani.

Ameongeza kuwa viziwi wanakabilwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na ukosefu wa ajira unaosababishwa na kushindwa kuelewana kati ya mtu mwenye ulemavu wa kusikia na mwajiri na kuiomba serikali kuwapeleka kwenye vyuo vya ufundi lli wapate ujuzi utakaowawezesha kujiajiri.

Mjumbe wa Chama hicho, Rehema Martin amesema kuwa ukosefu wa mkalimani katika Manispaa ya Kahama unasababisha wao kukosa taarifa mbalimbali na kupitwa na fursa nyingi za maendeleo ilhali Katibu wa Chama Cha viziwi,Kahama Clement Deogratius amesema kuwa wamekuwa wakipitwa na mafunzo mbalimbali kama namna ya kujikinga na maradhi kwakuwa hawana mkalimani wa kutafsiri Kwa lugha ya alama kile kinachozungumzwa.

Naye Afisa miradi wa Shirika la ushauri na udhibiti wa Ukimwi Kahama Dickson Joshua amesema kuwa pia kuna umuhimu kwa wananchi wa kawaida kujua lugha ya alama ili kurahisha mawasiliano kati yao na watu wenye ulemavu wa kusikia.

Wilaya ya Kahama ina zaidi ya watu mia moja wenye ulemavu wa kutosikia wanaotambulika rasmi katika Halmashauri ya Ushetu,Msalala na Kahama Manispaa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *