Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Victoria, kimeitaka Serikali kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio la kutekwa kwa Katibu wa Baraza la Vijana (BAVICHA) Mkoa wa Mwanza, Amani Mohammed anayedaiwa kutekwa na watu wasiojulikana Wilayani Misungwi februari 14, 2025.
Tamko hilo, limetolewa na Katibu wa chama hicho kanda ya Victoria, Zacharia Obadi wakati akizungumzia kuhusu tukio hilo la utekaji amesema watekaji waliwasiliana na rafiki yale wa kike ambaye walimuweka chini ya ulinzi ili asaidie kupatikana kwa katibu na baadae walivyompata walimchukua na kutokomea nae kusikojulikana.
Amesema, “tunashuhudia vitendo vya kihalifu vikiongezeka, hususan dhidi ya viongozi wa upinzani. Tunaitaka serikali kufanya uchunguzi wa kina na kuhakikisha ndugu yetu Amani Manengelo anapatikana salama.”

Kwa upande wao baadhi ya wanachama wa CHADEMA, wamelaani kukithiri kwa vitendo vya utekaji huku wakilitaka jeshi la polisi kuhakikisha kijana huyo anapatikana akiwa hai ambapo pia wamesisitiza uwajibikaji kwa vyombo vya usalama.
“tunahitaji haki na uwajibikaji wa vyombo vya usalama. Hatutakaa kimya hadi mwenzetu apatikane,” alisema mmoja wa wanachama hao Veronika Kunchu, huku Imelda Mafuru akiongeza kuwa, “Serikali ina jukumu la kulinda raia wake bila upendeleo wa kisiasa. Tunataka majibu, sio ahadi za uongo.”
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Audax Majaliwa amethibitisha kupokea taarifa za kutekwa kwa Kiongozi huyo, akisema uchunguzi unaendelea ili kuwabaini wahusika.
Hata hivyo, wanachama wa CHADEMA mkoani Mwanza hawajaridhishwa na hatua za awali zilizochukuliwa na wameazimia kuelekea katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, ili kushinikiza hatua zaidi zichukuliwe.


