Chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) kimesema kuwa kinatarajia kuzindua kampeni yake ya No reform No Election April 26 mwaka huu kanda ya Serengeti chini ya Mwenyekiti wa chama hicho Tundu Lissu.
Akiongea na waandishi wa Habari katibu wa CHADEMA Kanda ya Serengeti Jackson Mnyawani amesema viongozi wa chama hicho watapita katika majimbo yote 24 ya uchaguzi kanda ya Serengeti kuzungumza na wananchi ili kuwapa ujumbe wa mabadiliko kwenye mfumo wa uchaguzi nchini.

“Tutampokea mwenyekiti wetu wa chama april 26 na tutazunguka majimbo yote 24 ya uchaguzi kanda ya Serngeti kwa sasa Tupo kwenye hatua ya kuwashirikisha viongozi na wanachama ujumbe maalum kuhusu lengo letu kutaka mabadiliko kwenye uchaguzi ili kuhakikisha viongozi wanaokubalika wanachaguliwa na kutangazwa kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi” Amesema Mnyamani.

Kwa upande wake mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Kahama Mussa Bukango amesema lengo la kampeni hiyo ni kuhakikisha kunakuwa a uwiano wa wawakilishi kutoka kwenye vyama vyote ndani ya tume ili kushinikiza dhana ya haki na usawa huku akiwasihi wanachama wote kujitokeza kwenye mikutano yao.
“Lengo la hii operesheni ni kuhakikisha kila mtu anapata haki kwa mfano unamchagua mtu A na kweli matokeo yatoke kwa A aliochaguliwa siyo unamchagua A lakini matokeo yanatoka kwa B tunataka uwiano wa wawakilishi wa vyama ndani ya tume ili kuleta usawa,” Ameongeza Bukango.

Kwa upande wake Katibu mwenezi wa chama hicho jimbo la Msalala Prisca Nangawe amesema kuwa utekelezaji wa kampeni ya No reform No Election hailengi kuleta fujo bali ni kufikisha ujumbe kwa chama cha Mapinduzi na serikali iliyopo madarakani kuheshimu kura ya mtanzania.
“Kampeni hii haina lengo la kuhamasisha fujo bali tutawaeleza watu wetu kwanini uchaguzi usifanyike,tumeona katika uchaguzi wa serikali za mitaa uchaguzi ulifanya pasipokuwa huru na haki tutaenda kwa amani kabisa kuzuia uchaguzi usifanyike ili chama cha Mapinduzi na serikali yake ijue kwamba imefika hatua waiheshimu kura ya Mtanzaia” Amesema Nangawe.
