Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Kanda ya Serengeti inayo unganisha mikoa ya Mara, Simiyu pamoja na Shinyanga, wameunga mkono azimio la Chadema Makao Makuu, kwamba kama hutakuwa na mabadiliko hawata shiriki uchaguzi mkuu 2025, “No Reforms no Elections” huku wakiomba Serikali imwachie huru Mwenyekiti wao, Tundu Lissu.
Hayo yamebainishwa leo Aprili 16, 2025 na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Serengeti Lucas Ngoto, wakati akitoa tamko lao kwa waandishi wa habari,kikao kichofanyika katika ofisi za makao makuu ya kanda hiyo zilizoko Mjini Shinyanga.

Amesema uchaguzi ni Takwa la Kikatiba,ambapo wananchi wanapaswa kuchagua viongozi ambao wanawataka, lakini Katiba hiyo imekuwa ikikiukwa hasa Ibara ya 8, na uchaguzi kufanyika ndivyo sivyo, na ndiyo maana wanataka mabadiliko ya uchaguzi, ili uwe huru na haki na kupatikana wagombea kihalali na siyo kwa dhuruma.
Ngoto ametolea mfano uchaguzi wa serikali za Mitaa uliopita 2024, kwamba uligumbiwa na dhuruma nyingi,ikiwamo wagombea wao kuenguliwa kwa mapingamizi yasiyo na mashiko, na hata wale walioshinda uchaguzi huo baadhi yao kushindwa kuapishwa.

“kutokana na matukio ya dhuruma yalitokea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa uliopita, na tusipo kuwa imara yatatokea tena kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu,hivyo tuna ungana na viongozi wetu wa makao makuu kwamba “No Reforms no Election,” kama hakuna mabadiliko kamwe hatuwezi kushiriki uchaguzi 2025,” amesema Ngoto.
Aidha,wameiomba pia serikali imwachie huru Mwenyekiti wao wa CHADEMA Taifa Tundu Lissu na kwamba kuendelea kumng’ang’ani na kumpatia kesi ya uhaini huko ni kuogopa uchaguzi.

“Serikali isitake kututoa kwenye Agenda yetu ya kudai “No Reforms no Election” kwa kumkamata Mwenyekiti wetu Tundu Lissu na kumpatia kesi ya Uhaini, sasa hivi tutakuwa na Agenda mbili, No Reforms no Election na Free Tundu Lissu,” ameongeza Ngoto.
Katika hatua nyingine, amesema wao kutosaini Kanuni za maadili ya uchaguzi,siyo kwamba ndiyo wametolewa kutoshiriki uchaguzi, kwamba hakuna sheria inayosema Chama kisiposaini kanuni hizo hakitashiriki uchaguzi.

Naye Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Simiyu, Mussa Onesmo, amesema wanalaani tukio la kukamatwa Tundu Lissu, na kwamba watapeleka wanachama wao zaidi ya 100 Jijini Dar es salaam, kushinikiza aachiwe huru.
