CHADEMA IWASIKILIZE G55 – OLE NGURUMWA

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa amekishauri Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuketi meza moja na kundi la watia nia ubunge wa chama hicho, maarufu’ G55′ ili kumaliza sintofahamu iliyopo baina ya pande hizo mbili.

Sintofahamu hiyo imeibuka baada ya Chadema kushikilia msimamo wa ‘No Reforms No Election’ wakimaanisha bila mabadiliko, hakuna uchaguzi wakitaka serikali kufanya mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi.

Hata hivyo, kundi la G55 linaloundwa na makada waandamizi waliotia ubunge 2020 na 2025 linasema No Reforms sawa, lakini No Election haiwezekani kwa mazingira ya sasa huku wakitoa hoja sita za kutofautiana na hatua ya Chadema kutaka kuzuia uchaguzi.

Kutokana na mtanzuko huo, Ole Ngurumwa kupitia ukurasa wake wa mtandao X ameandika kuwa

“Nimefuatilia mjadala ndani ya Chadema, ninaandika kwa ufupi hapa lakini bado nitamtafuta Mhe Lissu (mwenyekiti wa Chadema).

Kabla ya kuendelea mbele katika andiko hilo, Ole Ngurumwa alikodeza kidogo historia ya miaka 30 kuhusu kundi G55 lililongozwa na wabunge akisema.

“Miaka zaidi ya 30 iliyopita wabunge wapatao 55 wakiongozwa na Njelu Kasaka waliunda kundi la wabunge G55 kwa lengo la kutaka kuonyesha kuna mambo hawakubaliani nayo ndani ya CCM na Taifa kwa ujumla likiwemo muundo wa Muungano.

“Wakapeleka hoja binafsi bungeni, baadaye Serikali iliunda kamati iliyoongozwa na Waziri wa Sheria( Hayati Samwel Sitta)pamoja na wajumbe wengine wakiwa (hayati Edward Lowassa,) Anne Makinda na (hayati DkSeif Khatib)

Kwa mujibu wa Ole Ngurumwa katika andiko hilo, amesema tume hiyo iliwasikiliza lakini hawakufikia mwafaka hadi Nyerere(Julius- hayati ) akawaita na kuwasilikiza wakiwa na Waziri Mkuu John Malecela.

Kuhusu G55 ya sasa

Ole Ngurumwa amesema enzi hizo cha chama kimoja walitoka watu na kutoa maoni yao ya kutaka kuwa na hoja binafsi, hivyo kuwepo kwa watu wenye mawazo tofauti ndani ya chama au Serikali hivi sasa ichukuliwe kama ni kukua kwa demokrasia na uhuru wa maoni.

“Nawashauri sana viongozi wa Chadema wa juu, tafuteni nafasi ya kuwasikiliza hawa wanachama wenu. Uongozi bora ni pamoja na kuwa na uwezo wa kutatua changamoto za ndani kwa kuwapa nafasi wenye maoni tofauti na kusikiliza hoja zao.”

Kwenye andiko hilo, Ole Ngurumwa ameongeza kuwa, “wengi tunapenda sana kuona utulivu katika vyama vya siasa kwa kuwa ndio njia pekee ambayo Watanzania wanaweza shiriki uongozi wa nchi,”

“Rafiki zangu Lissu , Heche (John ) Lema (Godbless) na Mnyika (John) tafuteni namna mkae na G55 yenu. Tupo tayari kusaidia majadiliano haya kati ya uongozi wa chama na G55 ili tuendeleze utamaduni wa mazungumzo pale tunapotofautiana kimitazamo,” amesema.

“Kuweni kitu kimoja na malizeni tofauti na msonge mbele kutafuta namna bora ya kuwa na uchaguzi huru na haki. Wengine tulishauri sana hili kabla ya uchaguzi wenu (uliofanyika Januari 21, 2025)

“Watanzania tujenge utamaduni wa kuheshimu watu wenye mitizamo tofuauti na kile unachomini.Kama tunavyoitaka serikali iheshimu wote wanapokuwa na mitizamo tofauti Serikali, vivyo hivyo iwe pia hata kwa vyama vya siasa,” amesema Ole Ngurumwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *