Chad Kufanya Uchaguzi wa Rais

Chad inafanya uchaguzi wa Rais leo Jumatatu Mei 6,2024 baada ya miaka mitatu ya utawala wa Kijeshi,uchaguzi ambao ni wa kwanza kwenye kanda ya Sahel tangu eneo hilo liliposhuhudia wimbi kubwa la mapinduzi ya kijeshi.

Uchaguzi huo ulipangwa kwa dhamira ya kuhitimisha miaka mitatu ya utawala wa mpito wa kijeshi chini Mahamat Idriss Deby aliyechukua madaraka mwezi April mwaka 2021 baada ya waasi kumuua baba yake Idriss Deby aliyekuwa kiongozi wa muda mrefu wa Taifa hilo.

Hata hivyo kura ya leo yumkini itaimarisha zaidi nafasi ya Mahamat kama mtawala wa taifa hilo na kuzima ndoto ya kufunguliwa milango ya demokrasia na kiongozi huyo anatarajiwa kupata ushindi ingawa mpinzani wake mkuu Succes Masra amekuwa akivutia wingi wa wafuasi kwenye mikutano ya kampeni kuliko ilivyotarajiwa.

Vituo vitafunguliwa mnamo saa moja asubuhi na kufungwa saa kumi na moja jioni. Raia milioni 8.5 wana haki ya kupiga kura kwenye uchaguzi huo wa leo na wanajeshi tayari walianza kupiga kura mapema siku ya Jumapili, matokea ya awali yakitarajiwa kutangazwa Mei 21 na matokeo kamili yatatolewa Juni 5 na iwapo hakuna mgombea atakayepata zaidi ya asilimia 50 ya kura, kutakuwa na duru ya pili ya uchaguzi Juni, 22.

Tangu alipomrithi baba yake kama kiongozi kwenye taifa hilo la Afrika ya Kati linalochimba mafuta, Deby ameendeleza uhusiano mzuri na Ufaransa ambayo ni mkoloni wa zamani wa Chad na mshirika wa muda mrefu katika wakati ambao tawala nyingine za kijeshi kwenye kanda ya Sahel ikiwemo Mali, Burkina na Niger zimeitaka Ufaransa na mataifa mengine ya magharibi kuondoa vikosi vyao kwenye mataifa yao

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *