Categories

Do you have a Story?

Call us on 0677 644 444 to submit your news story or incident report!

CCM Yatambia Miradi ya Kimkakati na Maendeleo Nchini

Na Eunice Kanumba,Shinyanga

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara John Mongella, amewataka wanachama wa chama hicho   kujivunia mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya Chama hicho kwa wananchi, chini ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwani tangu serikali ya awamu ya sita iingie madarakani miradi mingi ya maendeleo  na ya kimkakati imetekekelezwa katika maeneo yote hapa nchini.

Mongella ambaye pia ni mlezi wa chama cha Mapinduzi Mkoa wa Shinyanga, amebainisha hayo leo Septemba 6,2024 wakati akizungumza na wajumbe na viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Shinyanga Mjini.

Amesema kutokana na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kuitendea haki ilani ya uchaguzi wa Chama Cha mapinduzi (CCM,)na kutekeleza miradi mingi ya maendeleo kwa wananchi,  wana CCM wana kila sababu ya kujivunia chama cha Mapinduzi pasipo uoga kwani mafanikio yanaonekana kwa macho.

“Wana CCM tunakila sababu ya kutembea vifua mbele, kujivunia mafanikio ya utekelezaji wa ilani ya CCM kwa wananchi,sababu miradi mingi ya maendeleo imetekelezwa na mingine bado inaendelea kutekelezwa, na tusikae kimya kuitangaza miradi hii bali tuendelee kuinadi,”amesema Mongella.

“Hapa Shinyanga ni ngome ya chama cha mapinduzi CCM, na Mkoa huu unakwenda kupata mafanikio makubwa ya kimaendeleo, na miradi mingi imetekelezwa ambapo uwanja wa ndege Ibadakuli una historia ndefu lakini sasa unakwenda kukamilika, na pia kuna miradi mikubwa ya maji inatekelezwa,”ameongeza Mongella.

Aidha, amesema kutokana na utekelezaji wa ilani ya CCM kwa asilimia kubwa kwa wananchi, Chama hicho kinakwenda kushinda kwenye chaguzi zote.

 Naye mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa, akizungumza kwenye mkutano huo, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi mkoani humo kwa ajili ya utekelezji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Amesema shukrani ambayo watampatia Rais Samia kama mkoa wa Shinyanga, ni kumpatia ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka huu, na uchaguzi mkuu mwakani 2025.

“Maua ambayo tunampatia Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na kuleta fedha nyingi za miradi ya maendeleo hapa shinyanga, tutapiga kura za kujaa kwenye gunia la (rumbesa) na tunafurahi kutupatia walezi wa Chama ambao ni ngazi za juu”amesema Mabala.

Mongella yupo mkoani Shinyanga akiendelea na ziara yake ya kuimarisha uhai wa chama pamoja na kuzungumza na wananchi kwenye mikutano ya hadhara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *