CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimeagiza kurejeshwa kwa wagombea wote wa Udiwani ambao walipitishwa na Kamati za Siasa za Mikoa, pamoja na wale waliokuwa kwenye orodha ya awali waliyotumiwa Makatibu wa Mikoa wa CCM, ili wapigiwe kura za maoni upya, katika maeneo yao.
Taarifa iliyotolewa hii leo Agosti 1, 2025 na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi uenezi na mafunzo, CPA. Amos Makalla imeeleza kuwa hatua hiyo imetokana na uamuzi wa Kikao cha Sekreterieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, kilichofanyika Julai 31, 2025 ili kujadili kwa kina malalamiko yaliyotolewa katika maeneo mbalimbali nchini.

Sehemu ya Taarifa hiyo inaeleza kuwa, “Wagombea wote wa udiwani wa kata, waliopitishwa na Kamati za Siasa za Mikoa warejeshwe ili wakapigiwe kura za maoni. Wagombea wote waliopo kwenye orodha ya awali waliyotumiwa Makatibu wa Mikoa wa CCM, warejeshwe ili wakapigiwe kura za maoni.”
Kuhusu maelekezo yote yaliyotolewa awali, CCM imeeleza kuwa imeyafuta na hivyo Makatibu wa Mikoa wa CCM wote nchi nzima, wanatakiwa kuzingatia na kutekeleza maelekezo ya sasa.


