CCM WAZINDUA KAMPENI ZA UBUNGE KATAVI, WAGOMBEA WAKABIDHIWA ILANI

Na Daniel Gahu – Katavi.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Katavi kimezindua shughuli za kampeni Kwa wagombea wake ngazi ya ubunge na udiwani katika majimbo yote yanayopatikana ndani ya Mkoa huku kikiwakabidhi wagombea wake kitabu cha Ilani na kuwataka wajinadi kwa wananchi kupitia yale ambayo yameorodheshwa ndani ya ilani.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mikutano ya Kampeni kwa wagombea wa nafasi ya Ubunge na Udiwani, mgeni rasmi Gilbert Samnpa ambaye ni mjumbe wa Sekretarieti Kuu ya Chama cha Mapinduzi na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa chama kutoka Mkoa wa Katavi amesema ilani ya chama imebeba hoja za msingi ambazo zimelenga kuleta mabadiliko ya kimaendeleo katika majimbo, kata na vitongoji vyote ndani ya Mkoa wa Katavi.

Amewaomba wananchi wa Katavi kusikiliza sera zinazotokana na ilani ya chama Cha Mapinduzi na kuchukuwa jukumu la kikipigia kura za mafiga matatu yaani nafasi ya Rais, Ubunge na Udiwani.

“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya mambo mengi na mazuri ndani ya nchi yetu katika kipindi chake cha uongozi wa takribani miaka minne, alichukua nafasi ya kuliongoza taifa hili huku kila mmoja wetu akiwa katika sintofahamu ya mashaka kama ataweza kuliongoza taifa na kutuletea maendeleo, lakini cha kushangaza amefanya makubwa sana tofauti na matarajio ya wengi,” amesema Samnpa.

Kwa upande wake mgombea wa Ubunge Jimbo la Mpanda mjini kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi ndugu Haidary Hemed Sumry, amewaomba wananchi waepukane na minong’ono na maneno ya mitaani ya kutokuwa na imani juu yake na kuwaomba wampe imani naye atawalipa imani.

“Wakati nagombea nafasi ya udiwani mwaka 2020 Kata ya Makanyagio wananchi walio wengi hawakuwa na imani na mimi wakidhani bado ni kijana mdogo na muhuhuni, lakini baada ya kupata nafasi ya udiwani na kuchaguliwa kuwa Meya wa Manispaa ya Mpanda nimefanya mambo mengi na makubwa na kugeuka kuwa historia ndani ya Jimbo hili la Mpanda” amesema Haidary.

Aidha, naye mgombea wa Ubunge Jimbo la Nsimbo Mkoani hapa ndugu Anna Richard Lupembe amewaomba wananchi huku akiwa amepiga magoti wampigie kura za ndio ili awe mwakilishi wao tena kwa muhula mwingine ndani ya bunge ili akatekeleze sera zilizopo ndani ya Ilani ya chama na kuwaletea maendeleo yasiyo sahaulika katika jimbo la Nsimbo.

Nao wagombea wa nafasi ya udiwani kwa tiketi ya chama Cha Mapinduzi kutoka Kata zote za Manispaa ya Mpanda na Jimbo la Nsimbo wamewaomba wananchi kuwachagua katika zoezi la upigaji kura itakapofika tarehe 29 Oktoba kwani wao ndio mzizi wa maendeleo hivyo wananchi wanakila sababu ya kuwachagua.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *