Kuelekea mkutano maalum wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) taifa, kinatarajia kuzindua ilani ya uchaguzi ya mwaka 2025-2030 ambayo itatumika kunadi vipaumbele vyao katika kampeni za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi oktoba 2025.
Hayo yameelezwa leo Mei 24,2025 Jijini dodoma na Katibu wa itikadi, uenezi na mafunzo CCM, Amos Makalla wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mkutano huo utakaofanyika kuanzia mei 29 hadi mei 30, katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete.
“Tunauhakika tutaweka historia ya kuwa na mkutano wa kipekee kuvunja historia ya ule uliopita,maandalizi yamekamilika hata nyie Waandishi mnaona ukumbi unaendelea kupambwa sisi kila siku tunataka kufanya mambo ya kihistoria,” amesema CPA Makalla.

Aidha amesema kuwa mkutano huo utatanguliwa na kikao cha kamati Kuu ambacho kitafanyika Mei 26 na kisha Halmashauri Kuu Mei 28 .
Katika hatua nyingine,Makalla amesema kuwa Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano,Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuweka Jiwe la Msingi la Jengo la Makao Makuu ya CCM Mei 28 mwaka huu.
Amesema kuwa Jengo hilo litakuwa la kisasa ambalo litakuwa na huduma zote muhimu na litaendana na hadhi ya CCM ambayo kwa sasa inawanachama zaidi ya milioni 11.
“Tunajenga jengo la Makao Makuu pembeni ya Jengo hili ( Jakaya Conversion) ambalo litakuwa na facilities zote CCM ni Chama kikubwa Tanzania pamoja na Afrika,tumeona umefika wakati wa kuwa na jengo lenye facilities zote kumbi za mkutano, parking kwa sababu Chama hichi ni kimbilio la wananchi,” amesema Makalla.
Aidha amesema kuwa mkutano huo utakuwa na agenda tatu ambazo ni kupokea taarifa ya utekelezaji wa ilani ya CCM katika kipindi cha miaka mitano kwa Serikali zote mbili,uzinduzi wa ilani ya uchaguzi 2025-2030 na marekebisho madogo ya katiba.
“Nitumie fursa hii kuwaalika wajumbe wote wa mkutano Mkuu karibuni Dodoma mambo yote yamekamilika tunawakaribisha hata ambaye sio mwananchi hata kama hujaalikwa unakaribishwa pia tutaweka eneo maalumu kwa ajili ya kuangalia,” amesema.


