Simba Sports Club inatakiwa kulipa USD 85,000 baada ya kuadhibiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), katika matukio mbalimbali yaliyojitokeza kwenye mechi zao za Kimataifa.
Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally ameyathibitisha hayo hii leo Septemba 26, 2025 akisema adhabu hiyo itaambatana na kucheza bila mashabiki katika mchezo mmoja wa michuano ya CAF,
Faini ya USD 50,000 ilitokana na tukio la mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, dhidi ya Al Masry ya Misri ambapo shabiki alivamia uwanja na kusababisha usumbufu.

Aidha, baadhi ya mashabiki pia waliwasha moto maeneo ya jukwaani, kitendo kilichotafsiriwa na CAF kama tishio la kiusalama na ukosefu wa nidhamu.
Katika mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya RS Berkane ya Morocco uliofanyika katika uwanja wa New Amaani Complex Visiwani Zanzibar, Simba pia ilitozwa faini USD 35,000 kutokana na matukio ya vurugu na ukiukwaji wa taratibu za mchezo.


