Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere nchini Joseph Butiku amekemea vikali wimbi jipya la utekaji watu pamoja na mauaji huku akivitwika lawama vyombo vya ulinzi na usalama.
Taasisi ya Mwalimu Nyerere imetoa tamko hilo siku moja(Septemba 10,2024) baada ya aliyekuwa kiongozi wa chama kikuu cha upinzani Chadema Ali Kibao kuzikwa jana Jumatatu mkoani Tanga baada ya kutekwa na kisha kuuawawa jijini Dar es salaam.
Akizungumza na Waadishi wa Habari,Butiku amesema vitendo vya utekaji, unyanyasaji na mauaji siyo hulka ya Tanzania na kusisitiza kuwa taifa la Tanzania siyo taifa la wahuni wala wauaji bali ni taifa linaloendeshwa kwa kufuata misingi ya katiba na sheria zake.
Amesema ni muhimu Rais Samia akapewa taarifa sahihi na vyombo vya ulinzi na usalama na kuongeza kuwa licha ya kwamba suala la ulinzi na amani ya nchi ni jukumu la kila raia, lakini vyombo vyenye dhamana katika eneo hilo vinapaswa kuwajibika na kueleza kwamba vyombo hivyo vinajua yale yanayoendelea hivyo haviwezi kukwepa lawama na vinapaswa kuwajibika.
Tangu kuzuka kwa wimbi la utekaji na unyanyasaji vyombo vya ulinzi na usalama vimekuwa vikinyooshewa kidole cha lawama huku chama kikuu cha upinzani (CHADEMA) kimekuwa kikililaumu jeshi la polisi.
Mauaji ya kiongozi huyo wa Chadema yamelaniwa vikali na viongozi wa kisiasa, taasisi za kiraia pamoja na jumuiya ya kimataifa katika kpindi ambacho Ubalozi wa Marekani umehimiza kuwepo kwa uchunguzi wa kina ikisema vitendo vya namna hiyo havikubaliki katika uwanda wa demokrasia. Ubalozi wa Canada umeikaribisha hatua ya Rais Samia kuhimiza uchunguzi wa haraka juu ya tukio hilo.