Na Tryphone Odace, Buhigwe – Kigoma.
Shirika la Buhigwe Social Economic Development Organisation (BUSEDO) limezindua kampeni ya uhamasishaji wananchi kuhusu uhifadhi na utunzaji wa mazingira, ikiwa na lengo la kupunguza ukataji miti ovyo na uchomaji moto misitu, pamoja na kurejesha uoto wa asili katika vijiji na kata za Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma.
Uzinduzi wa kampeni hiyo umefanyika katika Kata ya Bukuba, ambapo BUSEDO imepewa dhamana ya kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira katika kata zote 20, vijiji 44 na vitongoji 192 vya Wilaya ya Buhigwe.
Mkurugenzi wa BUSEDO, Laurent Ntakimazi, alisema kampeni hiyo inalenga kuhakikisha jamii inakuwa mstari wa mbele katika kusimamia uhifadhi na utunzaji wa mazingira.

Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Kibuye, Kata ya Bukuba, Kabwito Mutale, alisema serikali ya kijiji inaendelea kusimamia sheria ndogo zinazolenga kukomesha uharibifu wa mazingira na uchomaji moto, huku hatua za kisheria zikichukuliwa dhidi ya watakaobainika kukiuka sheria hizo.
“Tuna sheria ndogondogo za usimamizi wa misitu na mazingira za kijiji naomba zifuatwe kwa kweli kumekuwa na changamoto ya uharibifu wa mazingira na hii inaleta adhari kubwa kwa maana vyanzo vya maji vinakauka kwahiyo tunaanza kusimamisa sheria na kuchukua hatua kwa wanaoharibu mazingira” alisema Mutale
Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe, George Mdege, amesema shughuli za kibinadamu zimekuwa miongoni mwa sababu zinazochangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji.

Amesema baadhi ya wananchi wamekuwa wakifanya shughuli za kilimo karibu na vyanzo vya maji, hali inayoweza kuathiri uhifadhi wa vyanzo hivyo na mazingira kwa ujumla.
Baadhi ya wawakilishi wa wananchi kutoka kata mbalimbali za Wilaya ya Buhigwe wameunga mkono kampeni hiyo, wakisisitiza kuwa elimu kwa jamii inapaswa kupewa kipaumbele ili kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira na kulinda rasilimali za asili.
Kampeni hiyo inatarajiwa kuendelea katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Buhigwe, ikilenga kuwafikia wananchi na kuwajengea uelewa kuhusu wajibu wao katika kulinda misitu, vyanzo vya maji na uoto wa asili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.


