Siku kumi baada ya kutangaza kujitoa katika jumuiya ya kiuchumi ya afrika Magharibi ECOWAS, Burkina Faso, Mali Na Niger zimetangaza kuwa, zinakusudia kujiondoa mara moja, licha ya kuwepo kanuni inayozitaka zibaki katika jumuiya hiyo kwa muda wa mwaka mmoja kabla ya kutekeleza rasmi uamuzi huo.
Kifungu cha 91 cha mkataba wa jumuiya hiyo ya kiuchumi ya nchi za magharibi mwa afrika kinaeleza kuwa nchi wanachama zitaendelea kubaki na wajibu wao kwa muda wa mwaka mmoja baada ya kuarifu kujiondoa kwao.
Lakini nchi hizo tatu, ambazo zote kwa sasa zinaongozwa na tawala za kijeshi zilizoingia madarakani kupitia mapinduzi, zimeamua kutosubiri hadi wakati huo.
Katika barua iliyotumwa na wizara ya mambo ya nje ya Mali kwa sekretarieti ya ECOWAS imeelezwa kwamba serikali ya jamhuri ya mali haifungwi tena na mpaka wa muda uliotajwa katika kifungu cha 91 cha mkataba.
ECOWAS ilichukua hatua ya kuiwekea mali vikwazo vikali wakati jumuiya hiyo ikijaribu kushinikiza kurejeshwa mapema kwa serikali ya kiraia na kuitishwa uchaguzi nchini humo.
Wizara ya mambo ya nje ya BURKINA FASO, nayo pia imetuma barua sawa na hiyo kwa ECOWAS, ikisisitiza kutekeleza uamuzi wa kujiondoa bila kuchelewa na usioweza kutenguliwa.
Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Magharibi mwa Afrika ECOWAS ilitazamiwa kufanya mkutano wa ngazi ya mawaziri mjini Abuja leo Alhamisi kujadili hali ya kisiasa na usalama katika eneo hilo.