BUNIFU ZINAZOZALISHWA ZISIISHIE KWENYE MAONESHO, ZIENDELEZWE – DKT. NCHEMBA

Wziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba ameitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na taasisi zake kuhakikisha bunifu zinazozalishwa na Watanzania haziishii kuonyeshwa kwenye maonesho, bali zinaendelezwa, zinalindwa na kupelekwa sokoni, ili zitoe suluhisho kwa changamoto mbalimbali na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Waziri Mkuu ametoa maelekezo hayo Agosti 24, 2026, jijini Tanga wakati akihitimisha Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu, akisisitiza umuhimu wa kujenga mfumo unaowawezesha wabunifu kubadilisha mawazo yao kuwa bidhaa na huduma zenye tija.

Amesema Tanzania ina wabunifu wenye uwezo mkubwa katika maeneo mbalimbali, hivyo hatua inayohitajika sasa ni kuhakikisha ubunifu huo unavuka hatua ya kuoneshwa kwenye maonesho na kufikia hatua ya kutumika, kuzalishwa kwa wingi na kuuzwa sokoni.

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema maonesho hayo yanaakisi jitihada za Serikali katika kutekeleza maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha elimu inayounganisha nadharia na vitendo, ili kuandaa wahitimu wenye ujuzi wa kujiajiri na kuingia kwa ufanisi katika soko la ajira.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Caroline Nombo amesema jumla ya taasisi 91 za umma na binafsi zimeshiriki katika maadhimisho hayo, ambayo yamehusisha maonesho ya elimu, sayansi, teknolojia na ubunifu, mashindano ya kitaifa ya ujuzi na ubunifu pamoja na makongamano yaliyolenga kujadili mchango wa elimu, ujuzi na teknolojia katika kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Mhe Husna Sekiboko amesema Bunge litaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali za kuendeleza elimu, ujuzi na ubunifu kupitia bajeti, sera na miongozo inayolenga kuwawezesha watafiti na wabunifu wa ndani kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Buriani amesema uwekezaji wa Serikali katika sekta ya elimu umeendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia mkoani humo na kuchochea mafanikio ya wanafunzi, huku akipongeza maonesho hayo kwa kuibua na kuonesha uwezo mkubwa wa Watanzania katika sayansi, teknolojia na ubunifu.

Kaulimbiu ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu mwaka 2026 ni “Elimu, Ujuzi na Ubunifu: Njia ya Kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *