Timu ya Soka ya Bunge la Tanzania, imeanza vizuri michezo ya 13 ya Mabunge ya Afrika Mashariki inayofanyika jijini Kigali nchini Rwanda, kufuatia ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya timu ya soka ya Bunge la Kenya.
Magoli ya Bunge Sports Club – Soka, yamefungwa na Jafary Chege (Mbunge wa Rorya), Simai Hassan (Mbunge wa Nungwi), Cosato Chumi Gaza (Mbunge wa Mafinga Mjini) na Ramadhan Billa (Mbunge wa Chakechake). Mchezo ukipigwa Uwanja wa Pele jijini Kigali.
Ushindi huo mnono umeifanya Bunge Sports Club – Soka, maarufu kama Tulia Boys kuongoza kwa kuwa na pointi tatu, wakifuatiwa na Bunge la Afrika Mashariki (EALA) na wenyeji Bunge la Rwanda ambao walitoka suluhu katika mechi ya ufunguzi.
Mapema leo mchezo kati ya Bunge la Uganda na Sudan Kusini haukuweza kufanyika baada ya kila timu kutuhumu kwamba kuna wachezaji ambao sio Wabunge kinyume na Kanuni ya Michezo inayotaka Washiriki kuwa Wabunge tu.
Akiongea na wachezaji wa Bunge SC -Soka Mwenyekiti wa Bunge Sports Club Abbas Tarimba amewapongeza wachezaji na akasikitika kwamba alitamani magoli yangekuwa 5-1, akikumbukia November 5.
Kesho ni zamu ya mchezo wa riadha, huku Bunge Sports Club – Soka ikitarajiwa kurejea tena uwanjani Jumatatu kucheza dhidi ya South Sudan muda wa saa 2:30 Asubuhi uwanja wa Pele.