BUNGE BONANZA KUWAKUTANISHA WATUMISHI WA UMMA

Na Gideon Gregory – Dodoma.

Takribani Wizara 14 na Taasisi zaidi ya 10, zinatarajiwa kushiriki Bunge Bonanza litakalofanyika kesho Jumamosi jijini Dodoma likilenga kuhamasisha mazoezi, kuimarisha afya na kujenga mshikamano miongoni mwa watumishi wa umma.

Mwenyekiti wa Bunge Sports na Mbunge wa Makete, Festo Sanga amesema hayo leo Agosti 28, 2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya bonanza hilo, akisema ushiriki wa taasisi mbalimbali unaifanya shughuli hiyo kuwa jukwaa muhimu la kuimarisha ushirikiano.

Sanga amesema bonanza hilo limepanua wigo wa ushiriki kwa kuwakutanisha watumishi kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali hatua inayosaidia kujenga mahusiano mazuri na mshikamano katika utumishi wa umma.

“Michezo ni sehemu muhimu ya kuimarisha afya za watumishi hasa katika kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, yakiwemo magonjwa ya moyo na figo ambayo yanaweza kuchangiwa na mtindo wa maisha usiozingatia afya,”amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa idara wa huduma za Serikali kutoka kwa wadhamini wakuu wa bonanza hilo, Vicky Bishubo amesema wanaendelea kushirikiana na Bunge na Serikali katika shughuli zenye manufaa kwa jamii, ikiwemo michezo.

“Tumeandaa vifaa mbalimbali kwa ajili ya bonanza hilo ikiwemo jezi, tracksuit, T-shirt, mipira, medali na makombe kwa ajili ya washindi huku tukiendelea kuhakikisha mazingira ya michezo yanakuwa salama na rafiki kwa washiriki,”amesema.

Bunge Bonanza linatarajiwa kuwakutanisha viongozi, wabunge na watumishi kutoka wizara na taasisi mbalimbali huku washiriki wakishindana katika michezo mbalimbali ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha afya bora, mshikamano na mahusiano mazuri katika maeneo ya kazi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *