BUKOMBE YAONGEZA MAKUSANYO MAPATO YA NDANI, UBUNIFU VYANZO VIPYA WAHIMIZWA

Halmashauri ya wilaya ya Bukombe Mkoani Geita imefanikiwa kufikia asilimia 139.80 ya ukusanyaji wa mapato ya ndani kutoka makadirio ya sh bilioni 4.36 hadi kukusanya sh bilioni 6.10 kwa mwaka 2025/26.

Aidha halmashauri hiyo imefanikiwa kuongeza makusanyo ya mapato ya ndani kutoka sh bilioni 3.73 kwa mwaka 2024/25 hadi kufikia Sh bilioni 6.10 mwaka 2025/26 sawa na ongezeko la asilimia 63.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Adelina Mfikwa alitoa taarifa hiyo katika mkutano maalum wa Baraza la Madiwani wa Kujadili Taarifa ya Hesabu za Mwisho za Serikali kwa mwaka 2025/26.

Alisema mafanikio hayo yametokana na uimara wa timu za ukusanyaji wa mapato, kuhuisha kanzidata za wafanyabiashara na biashara zao na kuimarisha matumizi ya Mfumo wa Malipo Mtandao (POS).

Alisema hatua hiyo imeongeza bajeti ya fedha za utekelezaji miradi ya maendeleo kwa mapato ya ndani kutoka Sh milioni 872 mwaka 2024/25 hadi sh bilioni 1.27 kwa mwaka 2025/26 sawa na asilimia 31.30.

Mweka Hazina wa Halmashauri ya wilaya ya Bukombe, Victory Mlowe alisema kwa mwaka 2025/26 walikusanya kutoka vyanzo vyake vya ndani, ruzuku kutoka serikali kuu na wahisani jumla ya sh bilioni 56.39.

“Kati ya makusanyo hayo kiasi cha shilingi bilioni 49.45 kimetumika kwa matumizi ya mishahara na matumizi mengineyo”, alisema Mlowe.

Mlowe alibainisha kuwa kwa mwaka 2025/26 miradi ambayo inaendelea ina thamani ya sh bilioni 13 ikiwemo ujenzi wa stendi, ujenzi wa soko, ujenzi wa jengo la utawala na miradi ya afya.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Bukombe, Erick Kagoma aliipongeza ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri kwa kufanya upembuzi yakinifu juu ya mapato na matumizi ya fedha za halmashauri hiyo.

Kagoma alisisitiza halmashauri kuendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato, ili iweze kupiga hatua mbele zaidi kila mwaka na kuongeza idadi ya miradi inayotekelezwa kwa mapato ya ndani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *