Na Clavery Christian – Bukoba.
Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba imeadhimisha siku ya Mazingira Duniani kwa kupanda Miti 500 ya Matunda katika Hospitali ya Wilaya.
Akifungua zoezi hilo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Dkt. Kisanga Makigo amezitaka Taasisi na watu binafsi kuendelea kupanda miti ili kuhifadhi mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

“Tumeamua kuchagua eneo hili la hospitali kwani lina uhitaji wa miti ya vivuli na matunda ili kuleta mwonekano na uboreshaji wa mazingira haya yanayotoa huduma za afya.”
Naye Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Dominic Ruta alisema Miti zaidi ya 500 imepandwa ikijumuisha Miparachichi na Michenza huku akisisitiza zoezi hili ni endelevu na miti mingine italetwa na kupandwa katika eneo hilo la Hospitali na maeneo mengine.

Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Halmashauri ya Bukoba, Elizaus Ezra aliushukuru uongozi wa Halmashauri kwa kuchagua kuja kupanda miti hospitalini hapo kwani watumishi na wagonjwa watanufaika kwa kupata matunda.
Siku ya mazingira Duniani huadhimishwa Juni 5 kila mwaka, ambapo kwa mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu imesemayo “Mazingira Yetu na Tanzania Ijayo,Tuwajibike Sasa,Dhibiti Matumizi ya Plastiki.”



