BUCHA BUBU CHANZO WIZI WA MIFUGO GEITA – JONGO

Na Frank Aman – Geita.

Jeshi la Polisi mkoani Geita, limesema moja ya kiini kikubwa cha ongezeko la matukio ya wizi wa mifugo mkoani humo ni uwepo wa mabucha bubu pamoja na biashara ya nyama na chakula isiyozingatia sheria.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi Mwandamizi (SACP Safia Jongo ametoa taarifa hiyo mbele ya Waandishi wa Habari na kuongeza kuwa pia wafanyabiashara wa chakula wanahusika.

Taarifa hiyo inakuja ikiwa ni siku chache tangu madiwani wa Manispaa ya Geita walipowasilisha malalamiko yao kuhusu tatizo hilo katika kikao cha Braza la Madiwani cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/25.

Kamanda Jongo ametaja wahusuka wakubwa wa matukio ya wizi wa mifugo wamebainika kuwa ni waharifu ambao waliwahi kufungwa lakini wakamaliza kifungo chao na wamerejea kufanya uharifu.

“Sisi kama jeshi la polisi tunaendelea kuwasisitiza wananchi, kujenga mazizi salama, kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi kwa maana ya sungu sungu ili tushirikiane kupambana na hao watuhumiwa.

“Lakini oparesheni mbambali zimepangwa ikiwemo kukagua mabucha kwa sababu mabucha haya bubu nayo yanachangia kuuza hizo nyama,” amesema Jongo.

Kamanda Jongo amewahakikishia wakazi wa Geita kuwa jeshi la polisi limeweka mipango thabiti kufuatilia kwa kina ili kuwadhibiti na kukomesha wizi wa mifugo na aina zote za uharifu.

Akizungumza katika Kikao cha Baraza la Madiwani Manispaa ya Geita, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Barnabas Mapande ameomba hatua za haraka zichukuliwe kudhibiti wimbi hilo.

Mapande amesema kwa siku za hivi karibuni wananchi wengi ambao ni wafugaji wilayani humo wanaishi bila amani na wameripoti kuibiwa mifugo yao na hivo vyombo vya ulinzi na usalama vitatue tatizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *