Huenda umewahi kusikia ndugu yako au rafiki yako au hata mpenzi wako akitafuna meno yake akiwa usingizini, tatizo ambalo huwapata takribani asilimia 1-30 ya watu katika jamii hasa watoto.
Tatizo hili la kusaga meno kwa kitabibu huitwa bruxism, na hali hii inaweza kusababisha meno kuharibika ikiwemo kupata matatizo mengine ya kiafya kwenye kinywa.
Kitengo hiki mara nyingi hufanyika wakati Mtu akiwa amelala, ingawa watu wengi (wahusika), huwa hawajui kama anasaga meno, lakini maumivu ya kichwa mara kwa mara au taya kuuma wakati unapoamka, huwa ni dalili kumpa utambuzi kuwa anasaga meno.

Hali hii huleta michubuko kwenye meno, kuleta hali ya ganzi, kulegea kwa meno, meno kung’oka na hata kupasuka na kusababisha pia madhara kwenye miunganiko ya taya la chini.
NINI SABABU?
Hali hii husababishwa na vitu kama msongo wa mawazo, hasira, magonjwa ya usingizi na shida ya kusaga meno sio tu kwa watu wazima pekee bali takriban asilimia 15 hadi 33 ya Watoto husaga meno.

Watoto ambao husaga meno yao hufanya hivyo kwa nyakati mbili (i) wakati meno yao yanapoota na (ii) wakati wanapoota meno ya kudumu na kwa kawaida watoto husaga meno wakati wa kulala.
Kwa mtoto sababu za kusaga meno ni pamoja na mawasiliano yasiyo ya kawaida kati ya meno ya juu na ya chini, magonjwa na hali zingine za kiafya (kama vile upungufu wa lishe, minyoo na mzio) na sababu za kisaikolojia ikiwemo wasiwasi.

MATIBABU
Daktari wa meno hutengeneza kitu kinaitwa mouth guard ambayo mgonjwa huvaa wakati wa usiku ili kuzuia kusaga meno, lakini pia mgonjwa hufundishwa namna ya kuepuka msongo wa mawazo ili asiweze kuendelea na hali hii.